Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Dakika tisini za mchezo wa mpira wa miguu zina kitu cha kipekee ambacho ni vigumu kukielezea kwa maneno ya kawaida, ni muda mfupi tu kwa kipimo cha saa, lakini ndani yake kuna furaha, huzuni, matumaini, hasira na mapenzi yasiyo na masharti, maana yake Soka si mchezo tu bali ni hisia, ni utambulisho, na kwa baadhi ya watu ni sehemu ya maisha yao ya kila siku.
Katika dunia ya leo, ni rahisi sana kusikia ndoa zikivunjika, Watu wanaapa kupendana milele lakini baada ya muda mfupi wanagawanyika kwa sababu mbalimbali Lakini jambo la kushangaza ni kwamba kwa mashabiki wengi wa soka, kuacha kuishabikia timu yao ni kitu kigumu zaidi kuliko hata kuvunja uhusiano wa kimapenzi.
Mashabiki wa soka wana mapenzi ya ajabu kwa timu zao, timu inaweza kupoteza mara nyingi, ikashuka daraja, au hata kukaa miaka mingi bila kombe, lakini bado mashabiki wake wanaendelea kuiunga mkono bila kuchoka, Watajazana viwanjani, watavaa jezi zao kwa fahari, na wataendelea kuamini kuwa siku moja ushindi utarudi.
Mfano mzuri ni mashabiki wa Arsenal waliokaa muongo miwili bila ubingwa lakini hawavunja uhusiano na timu yao, lakini uvumilivu wao msimu huu 2025/2026 unaweza ukazaa matunda kwani wamebakiza hatua chache kutwaa taji, Hali kama hii Inaonyesha Nini maana halisinya upendo kwenye Soka.
Ndani ya muda huo mfupi, mashabiki wanaweza kusahau matatizo yao ya maisha. Mfanyabiashara, mfanyakazi, mwanafunzi au dereva wa bodaboda wote wanakuwa kitu kimoja kushangilia timu zao, Wanashangilia pamoja, wanalia pamoja, na wakati mwingine wanabishana kwa nguvu zote wakitetea rangi zao.
Ni ajabu pia kuona kwamba mtu anaweza kuzaliwa na kurithi timu kutoka kwa baba yake, na baadaye akairithisha kwa watoto wake, Hapo soka linageuka kuwa urithi wa familia Si suala la ushindi pekee, bali ni uaminifu na mapenzi ya kudumu.
Dakika tisini zinapomalizika, matokeo yanaweza kuwa ushindi, sare au kipigo. Lakini kwa shabiki wa kweli, mapenzi hayaishii kwenye matokeo. Ataendelea kusema kwa fahari, “Hii ndiyo timu yangu.”
Ndiyo maana soka lina nguvu ya kipekee, Linaweza kuvunja mioyo kwa dakika moja na kuijenga tena dakika inayofuata, Linaweza kuwafanya watu wasiowahi kuonana wakumbatiane kwa furaha ya bao moja tu.
Kwa kifupi, dakika tisini za soka ni zaidi ya mchezo Ni upendo wenye hisia za kweli upendo ambao mara nyingi hudumu zaidi kuliko mahusiano mengi ya maisha.
0767915474,
lugembetimothy01@gmail.com





Post a Comment