Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Klabu ya Simba SC imetangaza kuanza kwa hatua mpya ya kihistoria baada ya kukamilisha maandalizi ya muda mrefu kuanzisha kampeni ya kutengeneza kadi maalum aina ya VISA zinazoifanya klabu kujiendesha kisasa kama Moja ya timu kubwa barani Afrika.
Kupitia taarifa rasmi, uongozi wa Simba umeeleza kuwa mradi huo umefanyiwa kazi kwa kipindi kirefu kutokana na unyeti na ukubwa wake, huku dhamira kuu ikiwa ni kuimarisha mifumo ya kisasa ya klabu na kuwapa wanachama thamani zaidi.
Bodi ya Wakurugenzi ya Simba imeweka wazi kuwa utekelezaji wa mradi huo utahusisha kampuni ya Mainstream Group, ambayo itaunda mfumo wa kisasa wa kiteknolojia, huku kampuni ya Nexus ikipewa jukumu la kutoa kadi hizo maalum kwa wanachama.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, kadi zitakazotolewa zitakuwa na sifa na ubora wa VISA, jambo linaloifanya Simba kuwa miongoni mwa klabu chache barani Afrika kuanzisha mfumo huo wa kisasa.
Mbali na kutumika kama kitambulisho cha uanachama, kadi hizo pia zitawezesha wanachama kuweka fedha, kufanya malipo mbalimbali na kushiriki miamala tofauti, hatua inayolenga kurahisisha huduma na kuongeza ushiriki wa wanachama katika shughuli za klabu.
Hatua hiyo inaonekana kuwa sehemu ya mkakati mpana wa Simba SC wa kujiendesha kibiashara kwa viwango vya kimataifa na kuendelea kujijengea hadhi kama moja ya klabu kubwa Afrika.
0767915474,
lugembetimothy01@gmail.com



Post a Comment