Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Morocco, Walid Regragui, ameamua kujiuzulu wadhifa wake kufuatia kushindwa kutwaa taji la Mataifa ya Afrika (AFCON) wakiwa katika ardhi ya nyumbani baada ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Senegal.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa, Regragui alichukua uamuzi huo mzito baada ya kutathmini mwenendo wa timu yake katika mashindano hayo, licha ya kuiongoza kufika hatua ya fainali, Kocha huyo aliamini kuwa ni wakati muafaka kuachia nafasi hiyo ili kutoa fursa kwa mabadiliko mapya ndani ya kikosi hicho.
Inaripotiwa kuwa kocha huyo tayari amewasilisha barua rasmi ya kujiuzulu kwa Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF), huku akieleza kuwa amejiuzulu kwa heshima na kwa maslahi mapana ya soka la taifa hilo.
Regragui ameondoka akiwa na miezi sita pekee kabla ya kuanza kwa michuano ya Kombe la Dunia, hali inayoliweka FRMF katika wakati mgumu wa kufanya maamuzi ya haraka kuhusu hatma ya benchi la ufundi.
Hadi sasa, FRMF bado haijatoa tamko rasmi kuthibitisha kuondoka kwa kocha huyo , hata hivyo vyanzo vya karibu na shirikisho hilo vimeeleza kuwa endapo kujiuzulu kwa Regragui kutathibitishwa, mchakato wa kutafuta kocha mpya utaanza mara moja
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com



Post a Comment