Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema Serikali imeamua kuendelea na Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Miguel Gamond, licha ya kupokea CV nyingi kutoka kwa makocha walioonesha nia ya kuinoa timu hiyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Februari 9, 2026, Makonda amesema Wizara kwa kushirikiana na mamlaka za soka nchini imejiridhisha na uwezo wa Gamond na kuona anastahili kupewa muda zaidi wa kuendelea na jukumu lake la kuinoa Stars.
“Tumepokea CV nyingi sana za makocha, lakini maamuzi ya Serikali ni kubaki na kocha ambaye tayari ameanza kazi, amewajua wachezaji na wao wamemfahamu, Gamond amepewa timu katika muda mfupi sana, lakini ameonesha uwezo wake,” amesema Makonda.
Ameongeza kuwa moja ya sifa kubwa ya Gamond ni uwezo wa kusoma mchezo, kufanya uchambuzi wa kina wa wapinzani kupitia video pamoja na kufanya mabadiliko yenye tija katika timu.
Makonda amesema Serikali ina imani kubwa na benchi la ufundi la Stars na kwamba lengo ni kuijenga timu imara itakayoweza kushindana kimataifa.
Kwa kauli hiyo, Gamond sasa anaendelea kuaminiwa kuiongoza Taifa Stars huku wadau wa soka wakisubiri kuona matokeo chanya zaidi katika michezo ijayo.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.


Post a Comment