KARIAKOO DABI: VITA ALAMA ZA UBINGWA

 

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Mchezo wa watani wa jadi kati ya Yanga na Simba utakaopigwa Machi 1, 2026 katika dimba la New Amaan , umechukua sura mpya huku presha ikiongezeka kwa upande wa Msimbazi baada ya matokeo ya hivi karibuni ya ligi.

Timu hizo zimecheza michezo 10 kila mmoja, ambapo Yanga wanaongoza kwa alama 28 kileleni huku Simba wakiwa na alama 23 nafasi ya tatu huku pengo la alama tano likiwa linawatenganisha.

 Kabla ya dabi ,Yanga waliweka wazi dhamira yao ya ubingwa kwa kuibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya JKT Tanzania, wakati Simba wakikwama kwa sare tasa ya 0-0 dhidi ya Dodoma Jiji.

Matokeo hayo yameufanya mchezo huu kuwa na shinikizo kubwa kwa Simba, Mnyama Endapo atashinda, atapunguza pengo hadi alama mbili na kurejesha matumaini ya kupigania taji, Lakini wakiteleza na kupoteza, pengo linaweza kupaa hadi alama nane hali itakayowafanya waanze kutoka taratibu kwenye ramani ya ubingwa.

Kwa upande wa Yanga, morali iko juu wakijivunia rekodi ya kushinda mara tano mfululizo dhidi ya mtani wao jambo linalowapa jeuri ya kuingia uwanjani wakiwa wanajiamini zaidi.

Wananchi wanaonekana “kushikilia roho ya mnyama”, wakiamini ushindi utazidi kuwapa mwanga wa kutetea taji lao.

Kariakoo Dabi ya safari hii si tu pambano la heshima ya mtaa, bali ni vita ya alama zenye uzito wa ubingwa, Macho ya mashabiki wa soka nchini sasa yataelekezwa kwenye dakika 90 zitakazoamua mwelekeo wa msimu kwa wababe hawa wa jadi siku ya Machi 1, 2026, New Amaan, Zanzibar.

0767915473

lugembetimothy01@gmail.com




0/Post a Comment/Comments