AZAM, DODOMA JIJI ZAKUMBANA NA ADHABU LIGI KUU

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imezitoza faini klabu za Azam FC na Dodoma Jiji FC kufuatia ukiukwaji wa kanuni mbalimbali katika michezo ya Ligi Kuu ya NBC, kwa mujibu wa maamuzi ya Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi yaliyotolewa Februari 11, 2026.

Katika Mechi Namba 082 iliyochezwa Dodoma, Dodoma Jiji ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons, klabu hiyo imetozwa faini ya Sh milioni tano kwa kosa la wachezaji wake kuchelewa kutoka chumba cha kuvalia kwa ajili ya kuanza mchezo.

Mbali na adhabu hiyo, Dodoma Jiji imepewa onyo kali kwa kosa la waokotaji mipira kuchelewesha makusudi urejeshaji wa mipira uwanjani, kitendo kilichotafsiriwa kama kupoteza muda, Pia klabu hiyo imeonywa kufuatia gari la matanga kuingia uwanjani wakati timu ikiendelea na mazoezi ya kupasha misuli kabla ya mchezo, tukio lililokiuka taratibu za uwanja.

Katika Mchezo Namba 048 iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, Azam FC nayo imetozwa faini ya Sh milioni tano baada ya wachezaji wake na baadhi ya viongozi wa benchi la ufundi kuingia uwanjani kwa kupitia lango lisilo rasmi (mita chache kutoka vyumba vya kuvalia) na kukanyaga kimiminika kilichokuwa kimewekwa eneo hilo, Kitendo hicho kililalamikiwa pia na timu pinzani, TRA United.

TPLB imesisitiza kuwa adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu ili kuhakikisha nidhamu, utaratibu na uendeshaji bora wa mashindano unazingatiwa wakati wote.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments