Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Klabu ya Young Africans SC imeweka wazi dhamira yake ya kupata matokeo chanya katika mchezo ujao hatua ya makundi mzunguko wa tano dhidi ya AS FAR Rabat utakaopigwa Januari 7, 2026 nchini Morocco.
Akizungumza kabla ya safari ya kuelekea Rabat, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, amesema kikosi kimejiandaa kisaikolojia na kimkakati, kikiwa na lengo moja la kupata matokeo chanya.
Kamwe alisisitiza kuwa Yanga haitazami mchezo huo kama mchezo mgumu bali wanauchukulia kama mchezo muhimu kwao kutokana na kuhitaji wao wa alama.
“Hatuendi kwenye mechi ngumu, tunaenda kwenye mechi muhimu, Mechi ngumu tulishamaliza dhidi ya Al Ahly, Dhidi ya AS FAR Rabat hatuna hofu wala wasiwasi, tunaenda pale kwa mentality ya kupata matokeo,” alisema Kamwe.
Aidha, Kamwe alibainisha kuwa uzoefu wa kikosi cha Yanga katika mashindano ya kimataifa umeimarika, jambo linalowapa ujasiri wa kucheza ugenini bila presha.
“Tumeondoka bila woga, hatujaacha mtu ofisini Kuna waliondoka jana, leo na wengine wataondoka kesho tunaenda wote ili kuhakikisha tunapambana hadi mwisho,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Kamwe, falsafa ya Yanga ni kutumia akili na uwezo walioujenga ndani ya uwanja. “Mentality ya Yanga ni kushinda popote, akili yetu inatutuma hivyo na uwezo tunao unatosha,” aliongeza.
Mchezo huo wa Januari 7 unatarajiwa kuwa wa ushindani mkubwa, huku Yanga ikilenga kuendeleza mwenendo mzuri na kujiweka kwenye nafasi nzuri katika kundi ili kuhakikisha wanatengeza mazingira mazuri kuelekea robo fainali.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.

Post a Comment