Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Klabu ya Real Madrid imeachana na kocha wake Xabi Alonso, uamuzi uliochukuliwa kwa makubaliano ya pande zote mbili, huku klabu hiyo ikimshukuru kwa mchango wake na kumuenzi kama mmoja wa mashabiki wakubwa wa Los Blancos kutokana na historia na mafanikio yake ndani ya klabu hiyo, akiwa mchezaji na kocha.
klabu imesisitiza kuwa uamuzi huo umefikiwa kwa heshima na maelewano, licha ya presha iliyokuwa ikimkabili Alonso kufuatia kipigo cha mabao 3-2 dhidi ya Barcelona katika fainali ya Supercopa ya Uhispania iliyochezwa Saudi Arabia.
Matokeo hayo yaliibua maswali mengi kuhusu mustakabali wa benchi la ufundi, na hatimaye yakawa mwanzo wa ukurasa mpya ndani ya klabu hiyo kubwa barani Ulaya.
Sambamba na hilo, Real Madrid imemtangaza Alvaro Arbeloa kuwa meneja mpya wa timu hiyo , kwa mara ya kwanza kabisa katika ngazi hiyo ya juu, bila kupitia hatua ya muda kama kocha wa mpito, Arbeloa, aliyekuwa akiinoa Real Madrid Castilla (timu B), sasa anapandishwa rasmi kuchukua nafasi ya Alonso.
Hatua hiyo inaonekana kama dhamira ya klabu kuendeleza falsafa ya kuamini watu waliokulia ndani ya utamaduni wa Real Madrid, Arbeloa ni mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, aliyewahi kuivaa jezi ya kifalme kwa mafanikio makubwa, na sasa anaaminiwa kuendeleza falsafa ya ushindani, nidhamu na ushindi.
Real Madrid imemshukuru Xabi Alonso kwa mchango wake na kumtakia kila la kheri katika safari yake ijayo ya ukocha, huku macho na matumaini yakielekezwa kwa Arbeloa, ambaye sasa anakabidhiwa jukumu zito la kuiongoza klabu hiyo katika Ligi Kuu ya Uhispania na michuano mingine barani Ulaya.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.


Post a Comment