Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Licha ya kutocheza ligi yao ya nyumbani kutokana na machafuko nchini Sudan, klabu ya Al Hilal Omdurman imeendelea kuonyesha uimara wa hali ya juu katika soka la Afrika.
Baada ya ligi ya Sudan kusimamishwa, Al Hilal imekosa makao maalumu, ikilazimika kutangatanga barani Afrika kutafuta ligi ya kucheza ambapo imeshacheza ligi ya Mauritania, na kwa sasa wanashiriki Ligi Kuu ya Rwanda.
Hata hivyo, changamoto hizo hazikuwavunja moyo, Kinyume chake, klabu hiyo imeendelea kujijenga na kuunda kikosi imara chenye ushindani mkubwa, kikionesha kiwango kisicho cha kawaida ukizingatia mazingira magumu wanayopitia kuwa mbali na mashabiki wao.
Katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Hilal wanaendelea kung’ara ambapo hadi sasa wamekusanya alama nane (8) katika Kundi C, Ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya vigogo Mamelodi Sundowns umeongeza heshima na hofu kwa wapinzani, huku alama nne (4) kati ya hizo wakizivuna dhidi ya mabingwa hao wa Afrika Kusini.
Kwa matokeo hayo, Al Hilal wamejikita kileleni mwa Kundi C, wakithibitisha kuwa hata bila ligi ya nyumbani, bila makazi ya kudumu, bado wana roho ya ushindi, nidhamu na uwezo wa kushinda Mataji.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com



Post a Comment