UBINGWA EPL UNAWATAKA ARSENAL WASHINDWE WAO TU

 

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Ligi Kuu ya England (EPL) msimu huu inaendelea kutoa picha ya kipekee, huku ishara zote zikionyesha kuwa ubingwa unajipendekeza kwa Arsenal hii ni baada ya michezo ya mzunguko wa 22 iliyopigwa wikiendi iliyopita, matokeo yamekuwa ya kushangaza na yenye faida kubwa kwa kikosi cha Mikel Arteta licha ya wao wenyewe kudondosha alama.

Arsenal wakiwa ugenini dhidi ya Nottingham Forest walilazimishwa sare tasa ya 0-0, matokeo yaliyowakatisha tamaa mashabiki waliotarajia ushindi ili kupanua wigo wa alama kileleni,hata hivyo, matokeo hayo hayakuumiza sana ndoto zao za ubingwa, kwani wapinzani wao wa karibu kwenye mbio hizo walipoteza alama zote tatu.

Manchester City walipoteza mchezo kwa kufungwa mabao 2-0 mbele ya Manchester United, wakati Aston Villa nao walipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Everton, Matokeo haya yamefanya kile kilichotarajiwa kutokea kupunguzwa kwa pengo la alama dhidi ya The gurners kushindikana kabisa.

Kwa sasa, pengo la alama kati ya Arsenal na Manchester City pamoja na Aston Villa limesalia kuwa pointi saba, hali inayoendelea kuipa Arsenal nafasi ya dhahabu ya kutwaa taji la EPL msimu huu.

Kinachoshangaza zaidi ni kwamba kila mara Arsenal wanapodondosha alama, wapinzani wao wakuu kwenye mbio za ubingwa nao hufanya hivyo hivyo, kana kwamba ubingwa unawasubiri vijana wa Emirates.

Hali hii inatoa ujumbe mzito, ikiwa Arsenal watashindwa kutwaa ubingwa msimu huu, basi hawatakuwa na wa kumlaumu zaidi ya wao wenyewe, Fursa zinaendelea kujitokeza, wapinzani wakijikwaa, na presha ikipelekwa moja kwa moja kwa Arsenal kuhakikisha wanazitumia nafasi hizo ipasavyo.

EPL inaendelea kuwa ligi ya ushindani mkubwa, lakini kwa msimu huu, dalili zinaonyesha wazi,ubingwa unawaita Arsenal, na ni juu yao kuamua kama wataitikia wito huo au la.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments