Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Hatimaye safari ya kuelekea AFCON 2027 imechukua mwelekeo rasmi baada ya nchi za Tanzania, Kenya na Uganda kukabidhiwa bendera ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kama ishara ya kupewa uenyeji wa mashindano hayo makubwa ya soka barani Afrika.
Hafla hiyo ya kihistoria ilifanyika mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa fainali ya AFCON kati ya Senegal na Morocco, ambapo Rais wa CAF, Patrice Motsepe, alikabidhi rasmi kijiti cha uenyeji kutoka Morocco kwenda kwa nchi hizo tatu za Afrika Mashariki.
Tanzania iliwakilishwa katika tukio hilo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, ambaye aliungana na viongozi wengine wa michezo kutoka Kenya na Uganda kupokea bendera ya CAF, hatua inayoashiria mwanzo wa maandalizi ya moja ya matukio makubwa zaidi ya michezo kuwahi kufanyika katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Uenyeji wa AFCON 2027 unatazamwa kama fursa adhimu kwa Tanzania, Kenya na Uganda kuonesha uwezo wao wa kuandaa mashindano ya kimataifa, kukuza uchumi kupitia utalii wa michezo pamoja na kuinua maendeleo ya soka katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa kukabidhiwa rasmi kijiti hicho, macho sasa yanaelekezwa katika maandalizi, huku mashabiki wa soka wakisubiri kwa hamu kuona Afrika Mashariki ikiandika historia mpya ya soka barani Afrika.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.

Post a Comment