SOLSKJAER YUKO TAYARI KUINOA UNITED

 

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Manchester United imeanza harakati za kumpata kocha mpya wa muda kufuatia uamuzi wa kumfuta kazi Ruben Amorim, hatua iliyochangiwa na matokeo mabovu pamoja na kauli zake zilizoonekana kuushambulia uongozi wa klabu hiyo kongwe England.

Uamuzi wa kuachana na Amorim umefikiwa baada ya United kuendelea kuyumba kwenye Ligi Kuu England na mashindano mengine, hali iliyoongeza shinikizo kutoka kwa mashabiki na wadau wa soka, huku uongozi ukiona kauli za kocha huyo dhidi ya mfumo wa uendeshaji wa klabu zikizidisha mgogoro wa ndani.

Katika hatua nyingine, taarifa zinaeleza kuwa aliyekuwa kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer, ameibuka na kuhitaji jukumu la kuinoa timu hiyo kwa muda, Solskjaer, ambaye aliwahi kuinoa United kwa mafanikio ya wastani kabla ya kuondoka, anaripotiwa kuonyesha utayari wa kurejea Old Trafford bila masharti magumu ya kifedha.

Chanzo cha karibu na kocha huyo wa Norway kinaeleza kuwa Solskjaer yuko tayari kusaini mkataba wa malipo ya msingi, huku maelezo mengine ya mkataba yakiwekwa kando, jambo linalotafsiriwa kama ishara ya mapenzi yake kwa klabu na dhamira ya kuisaidia katika kipindi hiki kigumu.

Manchester United bado inaendelea na vikao vya ndani kujadili hatima ya benchi la ufundi na inatarajiwa kutoa uamuzi wa mwisho ndani ya masaa kadhaa .

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments