SIMBA YAZIDI KUJIIMARISHA, CHAMA NDANI, BUDO HALI TETE

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Klabu ya Simba SC imeendelea kufanya mabadiliko kwenye kikosi chake katika dirisha dogo la usajili la mwezi Januari, ikiwa na lengo la kuimarisha timu kwa ajili ya mashindano ya ndani na kimataifa.

Rasmi, Simba imekamilisha usajili wa Ismael Toure beki wa kati raia wa Ivory Coast, aliyekuwa akiitumikia klabu ya Baniyas FC ya Falme za Kiarabu, Toure anatarajiwa kuimarisha safu ya ulinzi wa Wekundu wa Msimbazi kutokana na uzoefu wake wa kucheza soka la ushindani wa juu nje ya nchi.

Sambamba na hilo, Simba pia imemtambulisha rasmi Nickon Kibabage kuwa ni sehemu ya jeshi la Nyekundu na Nyeupe alitokea Singida black Stars hatua inayoashiria dhamira ya klabu hiyo kuongeza ubora na upana wa kikosi na ushindani wa nafasi katika maeneo mbalimbali ya uwanja.

Katika habari nyingine zilizoanza kutikisa, zinaeleza kuwa aliyekuwa shujaa wa klabu hiyo katika nyakati tofauti tofauti, Clatous Chama, tayari amesaini mkataba wa mwaka mmoja wa kurejea Msimbazi alitokea Singida black Stars, Hata hivyo, hadi sasa klabu bado haijatoa utambulisho rasmi wa kiungo huyo mshambuliaji, jambo linalowaacha mashabiki wakiendelea kusubiri kwa hamu kusubiri utambulisho wake.

Wakati huo huo, hatima ya Budo Mutale, kiungo wa Simba, inaelezwa kuwa ipo katika hali tete, baada ya jina lake kuingia kwenye hati hati za wachezaji wanaotarajiwa kutolewa kwa mkopo. Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni sehemu ya mpango wa klabu kupanga upya kikosi na kuwapa nafasi wachezaji wengine kupata muda zaidi wa kucheza.

Kwa ujumla, usajili wa Januari umeonyesha wazi kuwa Simba SC iko katika mkakati wa kurejesha ubora na ushindani wake, huku kurejea kwa Chama kukionekana kama kunukia kwa zama mpya Msimbazi, na kwa upande mwingine, baadhi ya wachezaji wakikabiliwa na mustakabali usioeleweka kadri dirisha la usajili linavyozidi kusogea mwisho.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com


0/Post a Comment/Comments