Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, ameonyesha kuthamini mchango mkubwa wa mashujaa wa timu ya taifa ya nchi hiyo kwa kuwazawadia fedha na viwanja vya kujenga makazi kufuatia mafanikio yao ya kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, kila mchezaji wa timu ya taifa ya Senegal atapokea zawadi ya Euro 115,000 (takribani Shilingi milioni 339 za Tanzania) pamoja na kiwanja cha mita za mraba 1,500 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba katika mji mkuu wa Dakar.
Sio wachezaji pekee waliokumbukwa, kwani pia kila mjumbe wa benchi la ufundi na shirikisho la soka la taifa watapatiwa Euro 75,000 (takribani Shilingi milioni 217) sambamba na kiwanja cha kujenga nyumba, kama sehemu ya kuthamini mchango wao katika mafanikio ya kihistoria ya taifa hilo.
Kwa ujumla, serikali ya Senegal imetenga jumla ya Euro 465,000 (sawa na takribani Shilingi bilioni 1.36) zitakazogawiwa kwa wadau wote waliokuwa sehemu ya safari ya ushindi wa AFCON, kuanzia wachezaji, benchi la ufundi hadi maofisa wa Wizara ya Michezo waliokuwa karibu na timu ya taifa.
Senegal ilitwaa taji hilo la AFCON baada ya kuwafunga wenyeji Morocco kwa bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliopigwa kwa ushindani mkubwa, ushindi uliothibitisha ubora na uimara wa Simba wa Teranga katika soka la Afrika.
Hatua hiyo ya Rais Faye imepokelewa kwa pongezi kubwa na wadau wa michezo barani Afrika, wakieleza kuwa ni mfano bora wa namna viongozi wanavyopaswa kuthamini mafanikio ya michezo kama chachu ya umoja wa kitaifa na motisha kwa vizazi vijavyo.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.


Post a Comment