MOROCCO NA SENEGAL WAKUTANA NA RUNGU CAF

 

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limetoa adhabu kwa timu za taifa za Senegal na Morocco kufuatia vurugu zilizojitokeza wakati na baada ya mchezo wa fainali Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.

Kwa mujibu wa maamuzi ya CAF, Kocha Mkuu wa Senegal, Pape Bouna Thiaw, amepigwa faini ya Dola za Marekani 100,000 (sawa na takribani Tsh. Milioni 255.5) kwa kosa la kuhamasisha wachezaji wake kutoka uwanjani kinyume na taratibu rasmi za mpira wa miguu.

Wachezaji wa Senegal, Iliman Cheikh Baroy Ndiaye na Ismaila Sarr wamefungiwa kila mmoja kucheza michezo miwili ya mashindano rasmi ya CAF, adhabu iliyotokana na utovu wa nidhamu dhidi ya mwamuzi wa mchezo huo.

Vilevile, CAF imelitoza Shirikisho la Soka la Senegal faini ya jumla ya Dola 600,000, ambapo Dola 300,000 (Tsh. Milioni 768) kwa kushindwa kudhibiti mashabiki wake, huku Dola nyingine 300,000 zikitolewa kama adhabu ya kushindwa kudhibiti nidhamu ya wachezaji na benchi la ufundi wakati wa mchezo huo.

Kwa upande wa Morocco, beki wao wa pembeni Achraf Hakimi amefungiwa kucheza michezo miwili ya CAF kwa kosa la uwanjani, Aidha, Shirikisho la Soka la Morocco limepigwa faini ya Dola 200,000 (Tsh. Milioni 511) kwa kushindwa kudhibiti wachezaji wake wakati wa mchezo.

Pia Morocco imepewa adhabu ya Dola 100,000 kwa kosa la utovu wa nidhamu kwa wachezaji na benchi la ufundi, ikiwemo kauli na vitendo vilivyolenga kuikashifu teknolojia ya VAR na mwamuzi wa mchezo.

CAF imesisitiza kuwa adhabu hizo ni sehemu ya jitihada zake za kulinda heshima ya soka la Afrika, kudumisha nidhamu na kuhakikisha mashindano yanaendeshwa kwa misingi ya haki, usalama na ustaarabu.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments