MADRID YAKUBALI KIPIGO NA TIMU DARAJA LA KWANZA

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Real Madrid imeendelea kuandamwa na nyakati ngumu baada ya kupoteza mchezo wa pili mfululizo, safari hii ikipigwa bao 3-2 na Albacete, timu inayoshiriki LaLiga 2 (Ligi Daraja la Kwanza) na inayoshika nafasi ya 17 kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Kipigo hicho kimeigharimu klabu hiyo kubwa barani Ulaya kuondoshwa rasmi katika hatua ya 16 bora ya mashindano ya Copa del Rey, jambo lililozua mshangao mkubwa kwa mashabiki na wadau wa soka.

Kabla ya kipigo hicho cha aibu, Madrid ilikuwa imetoka kupoteza 3-2 dhidi ya Barcelona, matokeo yaliyoashiria kuyumba kwa kikosi hicho , Hata hivyo, wengi hawakutarajia vigogo hao wa Hispania kushindwa mara nyingine , tena mikononi mwa timu ya daraja la pili.

Katika mchezo huo, Albacete walionyesha ujasiri, nidhamu na ari ya kupambana, wakitumia vizuri mapungufu ya safu ya ulinzi ya Madrid na kuadhibu kila kosa Licha ya Madrid kupambana kurejea mchezoni, juhudi zao hazikutosha kuokoa heshima wala ndoto ya kutwaa taji la Copa del Rey.

Matokeo hayo yamezua maswali mazito kuhusu uimara wa kikosi cha Real Madrid, maandalizi yao na mustakabali wao msimu huu, huku Albacete wakiandika historia kwa ushindi mkubwa dhidi ya moja ya klabu zenye mafanikio makubwa duniani.


0767915473

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments