Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Klabu ya Chelsea imetangaza rasmi kuvunja mkataba na kocha mkuu Enzo Maresca kwa makubaliano ya pande zote, uamuzi uliokuja wakati timu ikiwa bado inapambana kufikia malengo yake makubwa ya msimu katika mashindano mbalimbali.
Kupitia taarifa ya Chelsea , imemshukuru Maresca kwa mchango wake ndani ya klabu, akiongoza timu kutwaa mataji mawili muhimu ambayo ni UEFA Conference League pamoja na Kombe la Dunia la Klabu (FIFA Club World Cup), mafanikio yaliyoweka alama chanya katika historia ya karibuni ya klabu hiyo ya jijini London.
Kwa mujibu wa rekodi, Maresca aliiongoza Chelsea katika jumla ya mechi 92, akipata ushindi 55, amepiteza 25 sare 12 , huku akifanikiwa kutwaa makombe mawili makubwa katika kipindi chake cha uongozi. Licha ya takwimu hizo kuonesha mafanikio , uongozi wa klabu umeeleza kuwa mabadiliko ya kiufundi yameonekana kuwa muhimu kwa mustakabali wa timu.
Chelsea imesema kuwa, ikiwa na malengo makubwa ya kupambana katika mashindano manne ikiwemo kuhakikisha inafuzu kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya, pande zote mbili zimekubaliana kuwa mabadiliko ya benchi la ufundi yatatoa nafasi bora ya kurejesha timu katika mstari sahihi wa ushindani.
Hatua hiyo inaashiria mwanzo mpya kwa Chelsea huku mchakato wa kutafuta kocha mpya ukitarajiwa kuanza mara moja, Klabu imemtakia Maresca kila la heri katika maisha na kazi yake ya baadaye, ikisisitiza kuwa mchango wake utaendelea kukumbukwa na mashabiki wa The Blues.
0767815463,
lugembetimothy01@gmail.com.


Post a Comment