DJIGUI DIARRA AUTANGAZA UBORA WA LIGI KUU BARA KUPITIA AFCON 2025

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Kipa wa Yanga SC, Djigui Diarra, ameendelea kuitangaza vyema Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya kuonyesha kiwango cha bora katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 inayoendelea, akiiwezesha timu ya taifa ya Mali kufuzu hatua ya robo fainali.

Diarra amekuwa mhimili mkubwa wa mafanikio ya Mali katika hatua ya makundi, akionesha utulivu, uzoefu na uwezo mkubwa langoni uliosaidia timu hiyo kuvuka kuelekea hatua ya mtoano na hatimaye robo fainali, Kiwango chake kimevutia wachambuzi na mashabiki wengi wa soka barani Afrika, wakimtaja kama mmoja wa makipa bora kwenye michuano hiyo.

Jana, kipa huyo aliendelea kung’ara zaidi baada ya kuisaidia Mali kuiondosha Tunisia kwa mikwaju ya penati, kufuatia sare ya mabao 1-1 katika muda wa kawaida wa mchezo na 3-2 Katika hatua ya penati, Diarra aliokoa mikwaju miwili , hatua iliyothibitisha ubora wake na kuipa Mali tiketi ya kuendelea na safari ya AFCON 2025 ambapo watachuana na Senegal hatua ya robo fainali.

Kiwango bora Cha Diarra ni ushahidi tosha wa ushindani na ubora wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara , Mafanikio yake yameendelea kuipa heshima ligi hiyo kimataifa, yakionyesha kuwa ligi ya Tanzania ina uwezo wa kuzalisha na kuvutia wachezaji wa kiwango cha juu wanaoweza kung’ara katika majukwaa makubwa barani Afrika.

Kwa kiwango anachoendelea kuonyesha, Diarra si tu fahari ya Mali bali pia ni balozi muhimu wa soka la Tanzania, akithibitisha kuwa Ligi Kuu Bara ni jukwaa sahihi la kukuza vipaji na kuandaa wachezaji kwa mashindano makubwa ya kimataifa.


0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com




0/Post a Comment/Comments