Na Timothy Lugembe,
Mwanakwetu Sports
Ligi Kuu ya England (EPL) imeendelea kushika kasi baada ya michezo sita kupigwa katika viwanja mbalimbali, huku ushindani wa kuwania ubingwa ukiendelea kupamba moto.
Macho na masikio ya mashabiki wengi wa soka yalielekezwa kwa vigogo watatu wa ligi hiyo , Arsenal, Chelsea na Manchester United. Arsenal, maarufu kama The Gunners, wameendelea kuonyesha nia thabiti ya kulitwaa taji la EPL msimu huu baada ya kuicharaza Aston Villa kwa mabao 4-1.
Ushindi huo umekuwa wa muhimu kwa Arsenal kwani Villa ilikuwa inaingia kwenye mchezo huo ikiwa imeshinda michezo 11 mfululizo, rekodi iliyowafanya kuwa miongoni mwa timu zinazohofiwa msimu huu. Hata hivyo, Arsenal waliukata mtiririko huo na kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi, wakionyesha dhamira yao ya kutwaa ubingwa.
Kwa upande mwingine, hali si shwari kwa Chelsea na Manchester United ambao wameendelea kudondosha alama na kupotea taratibu katika mbio za ubingwa. Chelsea wamepoteza jumla ya alama nne baada ya kutoka sare katika michezo miwili mfululizo, ikiwemo sare ya mabao 2-2 dhidi ya Bournemouth.
Manchester United nao hawakuwa na bahati nyumbani baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Wolves, Licha ya Wolves kuonekana kuwa timu dhaifu kwa msimu huu, United walishindwa kutumia vyema faida ya uwanja wa nyumbani na kuondoka na alama tatu muhimu.
Matokeo hayo yanaendelea kuipa Arsenal nafasi nzuri ya kuendelea kuongoza ligi, huku Chelsea na United wakilazimika kurekebisha makosa yao mapema iwapo wanataka kubaki kwenye mbio za kuwania ubingwa wa EPL.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com




Post a Comment