TRUMP ATUNUKIWA TUZO MPYA YA AMANI YA FIFA, MASWALI YAIBUKA KUHUSU UTEUZI

 

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Rais wa Marekani, Donald Trump, ameibuka kidedea katika tuzo mpya ya amani iliyoanzishwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), tuzo iliyotolewa wakati wa hafla ya Droo ya Hatua ya Makundi ya Kombe la Dunia 2026 iliyofanyika Desemba 5, 2025 katika ukumbi wa Kennedy Center, jijini Washington D.C.

Tuzo hiyo mpya inayojulikana kama “FIFA Peace Prize Football Unites the World” imelenga kuwatambua watu waliochangia kuhamasisha amani, umoja na mshikamano kupitia soka, Kwa mujibu wa FIFA, walengwa wa tuzo wanatakiwa kuwa wale waliofanya matendo ya kipekee ambayo yameleta watu pamoja bila kujali mipaka ya mataifa au tofauti za kitamaduni.

Hata hivyo, pamoja na tuzo hiyo kupokelewa kwa hisia tofauti, swali kubwa limeibuka kuhusu mwenendo mzima wa uteuzi, Mpaka sasa FIFA haijaweka wazi vigezo vilivyotumika kumpendekeza wala kumchagua mshindi wake wa kwanza, jambo ambalo limeibua mjadala mpana miongoni mwa wadau na wachambuzi wa masuala ya uwajibikaji na uwazi kwenye taasisi kubwa kama FIFA.

Wachambuzi wa soka wanasema kuwa kutokuwekwa wazi kwa misingi ya tuzo hiyo kunatoa mianya ya maswali, hasa ikizingatiwa hadhi ya tukio pamoja na uzito wa ujumbe wa “amani duniani kupitia soka”.

Hata hivyo, kwa upande mwingine, tuzo hiyo inatajwa kuwa sehemu ya mkakati mpana wa FIFA kuendeleza ajenda ya kutumia soka kama daraja la kuunganisha mataifa kuelekea Kombe la Dunia 2026 litakalofanyika Marekani, Mexico na Canada.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments