Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
kiungo mshambuliaji nyota wa Liverpool, Mohamed Salah, ameibua sintofahamu baada ya kuashiria kuwa huenda mchezo dhidi ya Brighton ukawa wa mwisho kabisa kwake katika uwanja wa Anfield, wakati klabu hiyo ikiendelea kuporomoka kutokana na mfululizo wa matokeo mabovu.
Salah, ambaye amekuwa benchi katika mechi tatu mfululizo, amezua gumzo baada ya kauli zake zilizotolewa kupitia Viaplay, akisema amewataka wazazi wake kufika Anfield kushuhudia huenda ikawa ni heshima yake ya mwisho mbele ya mashabiki wa Liverpool.
“Niliwapigia simu wazazi wangu na kuwaambia waje kwenye mchezo wa Brighton, Sijui kama nitacheza au la, lakini nitaifurahia siku hiyo nitakuwa hapo kuwaaga mashabi kisha nitaelekea AFCON Kwa sasa sijui nini kinafuata,” alisema Salah.
Kauli hiyo imekuja katika kipindi ambacho Liverpool inapitia safari ngumu, ikipoteza muunganiko wa kiufundi na kushindwa kupata matokeo katika michezo yake ya hivi karibuni. Mashabiki wameonyesha wazi kutoridhishwa na kasi ya kuporomoka kwa timu huku maswali mengi yakielekezwa kwa benchi la ufundi kuhusu mustakabali wa mchezaji huyo.
Hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu Salah imeongeza mashaka zaidi ndani ya klabu, hasa ikizingatiwa kuwa ndiye mfungaji bora wa muda mrefu na mchezaji aliyekuwa mhimili wa mafanikio chini ya Jurgen Klopp kwa miaka kadhaa.
Licha ya sintofahamu hiyo, Salah alisisitiza kuwa atabaki na mapenzi ya dhati kwa klabu hiyo.
“Nitapenda na kuunga mkono Liverpool milele, mimi na watoto wangu hii itabaki kuwa timu yangu,” aliongeza.
Kwa sasa macho yote yataelekezwa kwenye mchezo dhidi ya Brighton, utakaopigwa Disemba 13 , ambao umegeuka kuwa tukio lenye hisia kali huku mashabiki wakijiandaa huenda kushuhudia mwisho wa enzi ya Mo Salah katika jezi nyekundu ya Liverpool.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.




Post a Comment