Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Klabu ya Simba Sports Club imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mzee Denis Prosper, ambaye ni baba mzazi wa mshambuliaji wa timu hiyo, Kibu Denis, taarifa kutoka ndani ya klabu zinasema kuwa Mzee Prosper amefariki dunia usiku wa kuamkia leo mkoani Kigoma.
Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na uongozi wa klabu hiyo yenye maskani yake jijini Dar es Salaam, Simba imetoa salamu za rambirambi kwa mchezaji wao Kibu Denis pamoja na familia nzima ya marehemu, ikiwahakikishia kuwa klabu ipo nao bega kwa bega katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.
“Simba inatoa salamu za pole kwa Kibu pamoja na familia nzima ya Mzee Denis kwa msiba huu mzito, na tupo pamoja katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, uongozi wa Simba umeomba Wanasimba wote na wadau wa michezo nchini kuwa pamoja na Kibu katika sala na maombi, ili apate nguvu ya kuvuka kipindi hiki kigumu na kurejea salama katika majukumu yake ya soka.
Marehemu Mzee Denis Prosper anatarajiwa kuzikwa kijijini kwao Kigoma, ingawa ratiba rasmi ya mazishi bado haijatolewa.
Simba SC imekuwa ikionyesha mshikamano mkubwa kwa wachezaji wake katika nyakati ngumu, na tukio hili linadhihirisha namna klabu hiyo inavyojali familia yake ya michezo.
Pumzika kwa amani mzee prosper.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.


Post a Comment