Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Je, wananchi wa Angola na mashabiki wa soka walihitaji nini zaidi kuthibitisha ukubwa wa tukio lao la miaka 50 ya Uhuru kuliko kumuona Lionel Messi akiwatoa hoi kwa ubora wake uwanjani?
Hilo ndilo swali lililoibuka baada ya Argentina kuichapa Angola 2-0 katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliochezwa Novemba 14 dimba la Novemba 11 jijini Luanda, kama sehemu ya maadhimisho ya nusu karne tangu taifa hilo lijikomboe kutoka kwa utawala wa Ureno.
Katika mchezo huo uliovuta maelfu ya mashabiki, nahodha wa Argentina Lionel Messi aling’ara kwa kufunga bao moja na kutoa pasi ya bao, akishirikiana vyema na mshambuliaji mwenzake Lautaro Martinez, aliyefungua ukurasa wa mabao dakika ya 43 kabla ya Messi kukamilisha kazi dakika ya 82.
Ripoti zinaeleza kuwa serikali ya Angola ililazimika kutoa takriban Dola milioni 13 ili kuwashawishi mabingwa wa Dunia 2022 kutua nchini humo kwa mchezo huu wa kihistoria, hatua iliyoonyesha namna tukio hilo lilivyokuwa la kipekee.
Mchezo huo uliiacha Angola ikijivunia kuukumbuka Uhuru wake kwa namna ya kipekee, huku mashabiki wakipata fursa adimu ya kushuhudia kipaji cha Messi kwa macho yao.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com



Post a Comment