Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Je, uteuzi wa Mtendaji mpya unaweza kuwa chachu ya safari mpya ya mafanikio kwa Azam FC? hilo ndilo gumzo jipya baada ya mabingwa hao wa zamani kutangaza mabadiliko makubwa katika safu ya uongozi.
Azam FC imemtangaza rasmi Mhispania Octavi Anoro kama Mtendaji Mkuu (CEO) mpya wa klabu hiyo, kwa mkataba wa miaka miwili utakaomweka katika wadhifa huo hadi mwaka 2027, Anoro anachukua nafasi iliyoachwa na Abdulkarim Nurdin ‘Popat’.
Taarifa iliyotolewa Novemba 14, 2025, imeeleza kuwa Anoro (42), anakuja Azam FC akiwa na rekodi pana ya kimataifa katika maendeleo ya utawala, biashara ya mpira wa miguu na mifumo ya kisasa ya uendeshaji wa klabu sifa ambazo Azam imeonekana kuzihitaji kwa muda mrefu ili kuongeza ushindani ndani na nje ya nchi.
Uongozi wa Azam FC umeeleza kuwa mabadiliko haya ni sehemu ya mpango mpana wa kuimarisha ubora wa klabu ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa, ikiwa ni ishara ya dhamira yao mpya ya kufanya vizuri zaidi baada ya misimu kadhaa yenye changamoto za ushindani dhidi ya vigogo wa soka la Tanzania.
Katika kuimarisha zaidi safu ya uongozi, Bodi ya Wakurugenzi pia imemteua Rashid Seif Mohamed kuwa Msaidizi wa Mtendaji Mkuu (Assistant CEO) Rashid ni mhitimu wa Master’s in Sports Management na ana ngazi ya pili ya ukocha kutoka Chama cha Soka England (FA), sifa zinazotarajiwa kuongeza nguvu katika usimamiaji wa kiufundi na kibiashara wa klabu.
Kwa ujumla, uteuzi wa viongozi hawa wawili unatazamwa kama hatua muhimu katika kupandisha ufanisi wa Azam FC, huku mashabiki wakisubiri kuona kama mageuzi haya yatarejesha makali ya klabu na kuifanya kuwa mpinzani hatari zaidi katika medani za soka la Tanzania na Afrika.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.


Post a Comment