Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) limeridhia ombi la klabu ya Fountain Gate kufanya usajili wa wachezaji wapya nje ya dirisha rasmi la usajili, kutokana na sababu za kiufundi zilizoikumba timu hiyo.
Awali, Fountain Gate ilikuwa imefungiwa na FIFA pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kufanya usajili kufuatia malalamiko ya wachezaji wawili wa kigeni waliokuwa wanadai malipo yao. Ili kuondolewa adhabu hiyo, klabu hiyo ilitakiwa kwanza kulipa madai ya wachezaji husika.
Mnamo tarehe 1 Septemba 2025, Fountain Gate ilikamilisha malipo ya mchezaji wa mwisho, na siku hiyo hiyo FIFA ikaondoa rasmi adhabu hiyo kwa barua maalum. Hata hivyo, licha ya kufunguliwa kwa adhabu hiyo, mfumo wa usajili wa FIFA haukufunguliwa kwa wakati, jambo lililosababisha klabu hiyo kushindwa kuwasajili wachezaji wapya hadi kufikia tarehe 7 Septemba 2025, siku ambayo dirisha la usajili lilifungwa rasmi.
Kutokana na hali hiyo, TFF iliandika barua maalum kwa FIFA ikiomba ruhusa ya dharura kuruhusu Fountain Gate kufanya usajili wa wachezaji wapya kutokana na changamoto ya kiufundi iliyokuwa nje ya uwezo wa klabu hiyo.
Baada ya kupitia maombi hayo, FIFA ilikubaliana na ombi la TFF, na kwa mujibu wa Kifungu cha 65(14) cha Kanuni za Ligi Kuu, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF ilikutana na kuidhinisha rasmi usajili wa dharura wa Fountain Gate mnamo 6 Oktoba 2025.
Uamuzi huo unaiweka Fountain Gate katika nafasi nzuri ya kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao wa mashindano, huku wadau wa soka wakitarajia kuona mabadiliko makubwa ndani ya timu hiyo
Taarifa hii imetolewa na Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania(TFF) kupitia kwa Ofisa habari na mawasiliano Clifford Mario Ndimbo.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.


Post a Comment