TAKWIMU KUELEKEA KUMPATA MVP

 


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Takwimu za msimu wa 2024/2025 zinaonyesha wazi kwamba mbio za kuwania tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu (MVP) wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara zitakuwa za kusisimua, huku majina ya Jean Charles Ahoua na Pacom Zouzoua yakipewa nafasi kubwa kutokana na mchango wao wa kipekee uwanjani.

Kwa mujibu wa rekodi rasmi

Jean Charles Ahoua, amekuwa silaha muhimu kwa kikosi chake Katika Ligi Kuu ya NBC pekee, amefunga mabao 16 na kutoa asisti 9, akichangia jumla ya mabao 25 katika michezo 28 Kati ya hayo, amefunga penalti 6 na mabao 2 ya mpira wa adhabu, akionyesha ubora wake kwenye mikwaju (mipira ya kutenga).

Katika Kombe la Shirikisho la CAF, Ahoua ameongeza mabao 3 na asisti 2, hivyo kufikisha jumla ya mabao 18 na asisti 9 msimu mzima, mchango wa mabao 27 katika mechi 34 alizoshiriki.

Kwa upande mwingine, Pacom Zouzoua naye hakuachwa nyuma Katika mechi 25 za Ligi Kuu, alifunga mabao 12 na kutoa asisti 11, akihusishwa moja kwa moja na mabao 23 ya kikosi chake.

Kwa takwimu hizo, Ahoua anaonekana kumiliki nafasi kubwa kwa kuwa na uwiano bora wa mabao na mechi nyingi zaidi, huku Zouzoua akionekana tishio kutokana na usawa aliouonyesha kati ya mabao na pasi za mabao.

Kwa wachambuzi wa soka, vigezo kama ubora wa mechi kubwa, nidhamu, na uthabiti wa kiwango msimu mzima vitakuwa na mchango mkubwa katika kumpata mshindi.

Tuzo hizi za heshima zinatarajiwa kutolewa mwezi Disemba, na mashabiki sasa wanasubiri kuona kama ni Ahoua mwenye moto wa mabao, au Zouzoua fundi wa pasi na magoli, atakayeibuka kidedea na kuandika historia kwenye tuzo ya MVP NBC Tanzania Bara.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments