Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Mkataba wa kiungo mshambuliaji hatari, Allan Okello (25) wa klabu ya Vipers SC na timu ya Taifa ya Uganda umebakiwa na miezi tisa pekee kabla ya kumalizika rasmi.
Kwa mujibu wa kanuni za soka, mara tu Januari itakapofika, Okello atakuwa huru kuzungumza na kusaini mkataba wa awali na klabu yoyote mpya, kwani itakuwa imesalia miezi sita tu kabla ya mkataba wake kumalizika, hii inamaanisha mchezaji huyo anaweza kuanza safari mpya ya soka nje ya Vipers kuanzia mwanzoni mwa mwaka ujao.
Licha ya tetesi zilizozagaa mitandaoni, imebainika wazi kwamba Yanga SC hawana mpango wowote kwa sasa wa kumsajili Allan Okello, habari zinaeleza kuwa viongozi wa Yanga hawajawahi hata kuingia mezani kwa mazungumzo na wawakilishi wa mchezaji huyo, jambo linalowafuta kabisa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania saini yake.
Okello ni mchezaji mwenye kipaji kinachovutia mashabiki wengi barani Afrika, hivyo tetesi za usajili wake zimekuwa gumzo kubwa hasa baada ya kuonyesha kiwango bora hapa karibuni kuanzia mashindano ya CHAN na sasa kufuzu kombe la dunia, ikumbukwe kwenye michezo miwili ya hivi karibuni na timu yake ya Taifa Uganda amefanikiwa kufunga kwenye Kila mchezo jambo linalothibitisha ubora wake.
Bila shaka, dirisha la usajili la januari linatarajiwa kuwa la moto zaidi, na jina la Allan Okello litakuwa miongoni mwa majina yatakayotikisa vichwa vya habari vya michezo hapa nchini.
Swali kubwa linalobaki ni: Je, atabaki Vipers, ataelekea Tanzania, au atasaka changamoto mpya sehemu nyingine barani Afrika au hata Ulaya? Mashabiki wanabaki na hamu kubwa kusubiri Januari ifike ili kuona hatma ya nyota huyo kijana ikichukua mwelekeo gani huku mashabiki wa Simba wakitamani zaidi kumuona akiwa kwenye rangi nyekundu na nyeupe.
0767915473
lugembetimothy01@gmail.com.
Post a Comment