MESSI AFUNGUKA KUHUSU HATMA YAKE KOMBE LA DUNIA NA KUSTAAFU

 


Timothy Lugembe

Mwanakwetusports.

Nahodha na gwiji wa soka duniani, Lionel Messi, ameweka wazi hisia zake kuhusu mustakabali wake wa kisoka baada ya mchezo wao hapo Jana dhidi ya Venezuela, akisisitiza kuwa ndoto yake kubwa ni kumalizia safari yake ya kandanda akiwa nyumbani, nchini Argentina.

Messi amesema kuwa licha ya kupata mapenzi na heshima kubwa katika kipindi chake kirefu akiwa Barcelona, bado alitamani zaidi kupata hisia hizo mbele ya mashabiki wake wa nyumbani.

“Kwa kweli kumalizia safari yangu hapa Argentina ni jambo ambalo nimekuwa naliota siku zote, Kumalizia nikiwa na watu wangu, Kwa miaka mingi nilipata upendo mkubwa Barcelona, lakini ndoto yangu kubwa ilikuwa ni kupata hali hiyo hiyo nyumbani kwangu,” alisema Messi.

Akizungumzia mafanikio na changamoto alizopitia akiwa na timu ya taifa, Messi alikiri kuwa safari yao haikuwa rahisi.

“Kwa miaka mingi mengi yalisemwa, lakini mimi nilichagua kushikilia mambo mazuri tuliyoyafanya pamoja na wenzangu, tulijaribu mara nyingi lakini tulishindwa kutwaa kila kitu, Baadaye ilitokea kwangu na kizazi chetu cha sasa, japokuwa pia baadhi ya wenzetu wa kizazi kilichopita hawakubahatika kushinda, hata hivyo, kila kitu tulichopitia kilikuwa cha kipekee na kizuri mno.”

Messi pia alizungumzia kuhusu nafasi ya kushiriki tena Kombe la Dunia, akisema kutokana na umri wake ni vigumu kuona akishiriki tena michuano hiyo.


“Kama nilivyosema awali kuhusu Kombe la Dunia, naamini sitashiriki jingine tena kutokana na umri wangu, jambo la kawaida kabisa ni kwamba sitaweza kufika huko Lakini sasa tupo hatua ya karibu, na hiyo inanipa msisimko na kunitia hamasa ya kulipigania kwa nguvu zote.”

Hata hivyo, alibainisha kuwa hana presha kubwa na anapenda kuishi maisha yake hatua kwa hatua.

“Kama ninavyopenda kusema kila mara, naishi siku kwa siku, mechi baada ya mechi hicho ndicho kitu ninachokizingatia kuendelea mbele hatua kwa hatua, kuangalia hali yangu na jinsi ninavyojisikia, ndipo naendelea kupigania ndoto hizi,” aliongeza Messi

Kauli hiyo ya Messi imeacha mashabiki wake wakiwa na hisia mseto furaha kutokana na mafanikio yake makubwa uwanjani, lakini pia simanzi kutokana na ukweli kwamba safari yake ya kipekee katika soka la kimataifa inakaribia ukingoni.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments