STARS YATAKATA MKAPA


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Katika mchezo wa ufunguzi ulioashiria mwanzo mzuri wa mashindano ya CHAN 2024, wenyeji Tanzania (Taifa Stars) waliibuka na ushindi wa mabao 2–0 dhidi ya Burkina Faso jana usiku katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Mechi hiyo, ambayo ilikuwa ni ya ufunguzi rasmi wa mashindano hayo ya wachezaji wa ligi za ndani barani Afrika, ilihudhuriwa na maelfu ya mashabiki walioufurahia ushindi huo wa heshima kwa Taifa huku pakichagizwa na burudani mbali mbali kutoka kwa wasanii kabla ya mchezo.

 Katika mchezo huo goli la kwanza la Stars lilifungwa na Abdul Suleiman “Sopu” kwa njia ya penalti dakika ya 45+3 baada ya mshambuliaji Clement Mzize kuangushwa ndani ya la hatari na beki wa Burkina Faso, Frank Tologo, Sopu aliweka mpira kimiani kwa utulivu na kuioa Stars uongozi.

Kipindi cha pili kilishuhudia Tanzania ikiendelea kulishambulia lango la wapinzani kwa kasi. Juhudi hizo zilizaa matunda dakika ya 71 baada ya Mohamed Hussein “Zimbwe jr” kufunga kwa kichwa safi kufuatia krosi ya Mudathir Yahya, Awali goli mwamuzi wa pembeni aliashiriabkuwa ni Offside lakini baada ya uhakiki wa VAR, likathibitishwa .

Takwimu zinaonyesha kuwa Taifa Stars walimiliki mpira kwa asilimia 63 na walifanya mashambulizi ya maana zaidi, wakipiga jumla ya mashuti 19 dhidi ya 8 ya Burkina Faso, huku safu ya ulinzi ya Tanzania ilikuwa imara chini ya nahodha Ibrahim Bacca.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikuwepo uwanjani kushuhudia pambano hilo, huku Rais Samia Suluhu Hassan akiwasilisha salamu za pongezi kwa kikosi hicho kupitia mitandao ya kijamii, akiwataka kuendelea kuipa sifa nchi kwenye mashindano haya makubwa.

Baada ya mchezo kutamatika Stars walijipatia kitita Cha shilingi Million 60, ambapo Millioni 20 kama goli la mama, Millioni 20 kutoka Waziri mwenye dhamana ya michezo Prof. Kabudi na million 20 kutoka kwa mkuu wa mkoa wa Dar es s laam Ndg. Chalamila Hali inayozidi kuongeza hamasa kwa wachezaji kuelekea michazo inayofuata.

Tanzania sasa inaongoza kundi lao kwa alama tatu, na wanaelekea katika mchezo ujao wakiwa na matumaini makubwa ya kutinga hatua ya mtoano, Kwa matokeo haya, Taifa Stars wameanza kampeni yao ya CHAN kwa kishindo, na mashabiki wa soka nchini wana kila sababu ya kuwa na imani na kikosi hicho.



0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments