Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Mkanganyiko mpya umeibuka kati ya watani wa jadi, Simba SC na Yanga SC, baada ya ratiba ya Ngao ya Jamii kutangazwa itachezwa Septemba 16, 2025, ambapo Simba hawakubaliani na ratiba hiyo jambo linaloibua kumbukumbu za misimu iliyopita ambapo michezo ya miamba hao iligubikwa na sintofahamu na malalamiko yasiyoisha.
Awali, mamlaka husika za soka zilikuwa zimetangaza kwamba mechi ya Ngao ya Jamii ingechezwa kati ya Septemba 11–14,hata hivyo, mabadiliko ya ratiba yaliyopeleka mchezo huo tarehe 16 yamewafanya Simba kulalamika kuwa hawatapata muda wa kujiandaa na mchezo wao wa kimataifa dhidi ya Gaborone United ya Botswana, uliopangwa kuchezwa Septemba 20, 2025.
Kwa mujibu wa ratiba, endapo Simba watashiriki Ngao tarehe 16, watatakiwa kusafiri kwenda Botswana siku inayofuata (tarehe 17), kisha kucheza mechi ya kimataifa siku ya Septemba 20. Viongozi wa Simba wamesema hali hiyo inawaweka kwenye wakati mgumu kutokana na uchovu wa wachezaji kitu ambacho kinawezankuathiri matokeo ya michezo wao.
Kwa upande wao, Yanga SC wamesema wako tayari kushiriki mchezo huo kwani ratiba yao ya kimataifa ipo Septemba 21, ikiwapa siku tatu za kupumzika kabla ya kurudi dimbani, hata hivyo, Yanga pia wameweka msimamo kwamba hawatakubali kucheza tarehe nyingine zaidi ya 16 lakini chini ya hapo wapo tayali.
Afisa habari wa klabu ya Yanga Ali Kamwe amenukuliwa akisema kuwa wapo tayali kubadili ratiba yao ya wiki ya wananchi na kuifanya kuwa Ngao ya jamii ili kuisaidia jamii inayowazunguka, hivyo kama Simba wapo tayari waende.
"Sisi tupo tayari kuibadilisha Wiki ya Mwananchi iwe mechi ya Ngao ili tuweze kuisadia jamiii, hivyo kama kuna shida ya tarehe basi tarehe 12 ipo na Yanga tupo tayari tutawastopisha Bandari FC halafu mtani ambae hatumii hata gharama ya ndege kuja basi aje kwa Mkapa." Alisema Ali Kamwe.
Mkanganyiko huu unarejelea hali kama iliyojitokeza msimu uliopita ambapo michezo ya watani wa jadi ilitawaliwa na malalamiko ya uchezeshaji na upangaji ratiba, jambo lililoacha mashabiki na wadau wa soka katika mvutano wa muda mrefu.
Wachambuzi wa soka wanaona kuwa hali hii ni kielelezo cha changamoto za upangaji wa ratiba ndani ya soka la Tanzania, wakisisitiza kuwa Shirikisho la Soka (TFF) na Bodi ya Ligi wanapaswa kusimamia kwa umakini zaidi mechi kubwa kama hizi ili kuepusha malalamiko yanayoweza kuathiri ushindani na hadhi ya michuano.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.
Post a Comment