NAHODHA WA TWIGA STARS ATUA SPAIN

 

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Mshambulizi hatari wa Timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania, Twiga Stars, Opah Clement, ameanza ukurasa mpya wa maisha yake ya soka baada ya kutangazwa rasmi kujiunga na kikosi cha SD Eibar Women kinachoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake nchini Hispania.

Opah ametua Hispania akitokea klabu ya Juarez Femenil ya Mexico kama mchezaji huru, hatua hiyo inamfanya Opah kuwa Mtanzania wa kwanza kushiriki Ligi Kuu ya Wanawake Hispania na wa pili kucheza ligi kubwa barani Ulaya baada ya Mtanzania Aisha Masaka, anayewakilisha klabu ya Brighton katika Ligi Kuu ya England.

Nahodha huyo wa Twiga Stars mwenye umri wa miaka 24, amewahi pia kulitumikia vilabu mbalimbali barani Afrika, Asia na Ulaya ikiwemo Simba Queens (Tanzania), Kayseri Kadin na Besiktas (Uturuki) pamoja na Henan Jianye ya China.

Safari ya Opah ni chachu ya mafanikio kwa wanasoka wa kike nchini Tanzania, huku wadau wengi wakiamini kwamba hatua hiyo itafungua milango zaidi kwa vipaji vipya kuonekana kwenye ramani ya soka la kimataifa.

Soka la wanawake nchini Tanzania linazidi kukua kwa nyanja tofauti tofauti ikiwemo kutoa vipaji nje ya nchi pia wachezaji wa kigeni kutoka nje ya Tanzania wamekuwa wakivutiwa kujiunga kucheza katika ligi hiyo kitu ambacho kinazidi kulikuza soka la wanawake nchini, na hii yote ni matunda ya uwekezaji kutoka kwa Shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF).

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments