JE, UBORA WA LIGI NI UWEZO WA TIMU ZA TAIFA?

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Mashindano ya CHAN2024 yamatamatika rasmi siku ya Jana baada ya Kupigwa kwa mchezo wa fainali uliowakutanisha Madagascar vs Morocco ambapo timu ya Taifa ya Morocco wakiibuka mabingwa kwa mara ya tatu kwa ushindi wa mabao 3-2 katika uwanja wa Moi International Sports Center,Nairobi Kenya.

Baada ya mashindano hayo mjadala mkubwa uliibuka kuhusu iwapo ubora wa ligi za ndani ndio unaojenga nguvu ya timu za taifa, michuano ya CHAN 2024 imeibua mjadala huo kwa namna ya kipekee, baada ya mataifa ambayo hayana ligi kubwa zenye ushindani kufanya vizuri na kufika katika hatua za juu kabisa katkika mashindano .

Nchi kama Madagascar, Sudan na Senegal zimekuwa mfano bora katika michuano hiyo, Wachezaji wao, wameonesha ubora mkubwa licha ya ligi zao kutokuwa na ubora ukilinganisha na nchi nyingine, kilicho shangaza wadau wengi wa soka ni timu ya taifa ya Sudani kushika nafasi ya tatu ilihali nchini mwao hakuna ligi inayo chezwa kutokana na machafuko yanayo endelea nchini humo.

Timu hizo zimefanikiwa kutokana na nidhamu, morali ya hali ya juu, ubunifu, uzalendo na uwekezaji katika soka la vijana uliopelekea matokeo ya kushangaza, timu hizo ambazo hazina ligi zenye ushindani wamewashangaza wengi kwa ushindani uliotukuka kufanya vizuri tofauti na matarajio.

Kwa upande mwingine, mataifa yenye ligi zenye majina makubwa , miundombinu mizuri na uwekezaji mkubwa kama Tanzania,Nigeria na Algeria yalipata wakati mgumu kwa kutoka mapema katika mashindano hayo, jambo lililoacha maswali mengi vichwani mwa wadau wa soka ukilinganisha ubora wa ligi zao.

Wataalamu wa soka wanasema mafanikio ya timu ya taifa hayategemei tu hadhi ya ligi, bali pia nidhamu ya wachezaji, mfumo wa ufundishaji, uwekezaji wa muda mrefu katika vijana na mshikamano wa kikosi, CHAN 2024 imedhihirisha kuwa hata wachezaji wa ligi za kawaida wanaweza kung’ara kimataifa iwapo watapata malezi mazuri na kuandaliwa kwa umakini kwa kuzingatia misingi ya soka.

Mafanikio ya timu ya Taifa kama vile Madagascar wamefanikiwa kuonyesha ushindani mkubwa kutokana na miradi mbali mbali ya maendeleo ya michezo ikiwemo kuanzisha Accademy za michezo na na kutengeneza vipaji na kuviendeleza na kuwafanya wafanye vizuri katika timu ya taifa.

Hali hii inatoa funzo kubwa kwa mataifa yanayotegemea majina makubwa ya ligi badala ya kuwekeza katika maendeleo ya wachezaji chipukizi na mipango ya muda mrefu, ni wazi kuwa kiwango cha ligi ni nyenzo muhimu, lakini si kipimo pekee cha mafanikio ya timu ya Taifa kinachotakiwa ni uwekezaji kwenye soka la vijana kwa kutengeneza academy na kuendeleza vipaji kuanzia mashuleni na kuingia mtaani kutafuta vipaji na kuwapatia nafasi katika ligi zetu.

CHAN 2024 imeacha ujumbe mzito kuwa Ushirikiano, nidhamu na mipango endelevu huzaa matunda bila kujali nafasi ya ligi zetu, hivyo basi shirikisho la mpira wa miguu Tanzania kwa kushirikiana na bodi ya ligi wanayo kazi ya kuhakikisha wanaazisha program mahususi za kuibua vipaji vya vijana na kuwaingiza kwenye Academy na kuendeleza vipaji vyao.

Vipaji hivyo vitadumu na kukua kwa kuwepo na ligi maalumu za vijana ambazo zitachukua mzunguko mkubwa ili kuwapa vijana uwezo na kujiamini, na sio kama wanavyo fanya sasa ligi ya vijana inachezwa chini ya mwezi mmoja bingwa anapatikana baada ya hapo hatuelewi vijana wale wameishia wapi.

Eneo la mwisho linatakalo ifanya timu ya Taifa ifanye vizuri ni ushirikiano kutoka kwa mashabiki , waTanzania wengi wamechagua kuzishangilia Simba na Yanga na kuisahau timu ya Taifa hivyo basi ni wakati wa watanzania kuishika timu ya taifa mkono kwa kuipa hamasa itakapo kuwa ikicheza ushirikiano ukiwepo lazima timu ya Taifa itafanya vizuri.

Kitu cha muhimu inabidi tutambue kuwa ubora wa ligi sio ubora wa timu za Taifa kwa sababu ligi inaweza kuwa bora kutokana na uwekezaji ambao unawafaidisha wachezaji wa kigeni Zaidi lakini wazawa ambao wanaunda timu ya Taifa wanapata nafasi kwa uchache mfano mzuri ikiwa ni timu ya Taifa ya Uingereza licha ya ubora wa ligi yao na uwekezaji mkubwa lakini timu yao haifanyi vizuri .

Suluhu ni kuwapatia wachezaji wetu nafasi na kupunguza idadi ya wacheaji wa kigeni au katika kila mchezo iwekwe sheria wachezaji wa kigeni wanaotakiwa kucheza mfano, wasizidi watano hapo kwa kiasi Fulani tunaweza kupiga hatua.

0767915473,

Lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments