Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Kiungo nyota wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) na Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto' ameongeza mkataba wa mwaka mmoja na klabu hiyo ya Chamazi, hatua inayomfanya kubaki klabuni hapo hadi mwaka 2027.
Awali, Fei alikuwa na mwaka mmoja pekee wa mkataba uliobaki, lakini amesaini nyongeza ya mwaka mmoja na Azam, akiweka rekodi mpya ya kuwa mchezaji wa Kitanzania anayelipwa kiasi kikubwa zaidi nchini.
nyongeza ya mkataba huo umeambatana na ofa lukuki ikiwemo ,Malipo ya kusaini (Sign on fee) Fei amepokea shilingi milioni 800 taslimu, Mshahara wa kila mwezi atakuwa akipokea shilingi milioni 50 baada ya makato ya kodi pia Ubalozi wa Azam Pesa atalipwa shilingi milioni 200 kwa mwaka kupitia mkataba wa ubalozi.
Aidha, Azam FC imepandisha thamani ya kipengele cha kumuuza kutoka dola za Kimarekani 500,000 hadi 800,000, hatua inayoongeza ugumu wa klabu nyingine kumsajili akiwa ndani ya mkataba.
Kwa uamuzi huu, ndoto za Simba SC kumsajili Fei Toto msimu huu zimezimika rasmi, baada ya majaribio yao kushindikana kufuatia Azam kuwekeza fedha kubwa kuhakikisha nyota huyo anaendelea kuwatumikia.
Misuli ya kifedha ya Azam fc ndio imekuwa silaha kubwa kwa kuweza kumbakiza mchezaji huyo katika timu Yao, hatua hii imekuja baada ya shinikizo la kocha mpya wa klabu hiyo kuomba Fei asiuzwe Kwani alikuwa na malengo naye na ombi lake limeshughulikiwa hatimaye Fei amesalia klabuni hapo hadi 2027.
Mashabiki na wadau wa soka nchini walitamani Feisal atafute changamoto nyingine huku njia pekee ambayo ingeuza jina lake na kumtambulisha kimataifa ilikuwa ni kujiunga na wekundu wa msimbazi, kwani klabu hiyo inahistoria kubwa kwa kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
Swali la kujiuliza ni je, Fei ameridhika kucheza nchini, na ndoto zake kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania zipoje , na je, Azam fc ni mahali sahihi kwa yeye kuonekana kimataifa?
0767915473.
lugembetimothy01@gmail.com.
Post a Comment