Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Kwa mara ya kwanza tangu ajiunge na Simba SC, beki kisiki wa pembeni Mohamed Hussein "Zimbwe Jr" ameondoa jina la klabu hiyo kwenye wasifu wake wa mitandao ya kijamii, hatua inayozua maswali mengi kuhusu hatima yake katika klabu hiyo yenye mashabiki wengi nchini.
Zimbwe kwa sasa ni mchezaji huru baada ya mkataba wake na Simba kumalizika bila kusainiwa upya, Hadi sasa hakuna taarifa rasmi kutoka kwa uongozi wa Simba SC juu ya mustakabali wa mchezaji huyo, hali inayoacha mashabiki na wadau wa soka katika sintofahamu.
Mohamed Hussein, ambaye amekuwa tegemeo kubwa katika kikosi cha Simba kwa misimu kadhaa, ameisaidia klabu hiyo kunyakua mataji kadhaa ya Ligi Kuu ya NBC, FA Cup, na kufika hatua za juu katika mashindano ya kimataifa kama Ligi ya Mabingwa Afrika, Uwezo wake mkubwa wa kucheza nafasi ya beki wa kushoto kwa kasi, kupiga krosi zenye macho, na uimara wa kukaba, vimemfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wa kuaminiwa ndani ya klabu hiyo.
Zimbwe Jr mpaka sasa ameitumikia Simba kwa zaidi ya miaka 15, na ndio mchezaji mkongwe klabuni hapo kuondoka kwake kitakuwa pigo kwa klabu kwani amekuwa ni mchezaji imara ambaye hasumbuliwi na majeraha hovyo.
Swali la kujiuliza ni Je, huu ndio mwisho wa safari ya Zimbwe ndani ya Msimbazi? Je, ataelekea timu gani msimu huu? Haya ni maswali yanayosubiriwa kwa hamu na wadau wa soka nchini na majibu yake yatapatikana siku za usoni.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.
Post a Comment