Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Klabu ya Yanga SC imeendelea kuonyesha nguvu yake kwenye dirisha la usajili kwa kufanikisha dili la kiungo chipukizi wa kimataifa kutoka CS Sfaxien ya Tunisia, Mussa Balla Conte (21) siku tano zilizopita, baada ya Simba SC kushindwa kumaliza dili hilo kutokana na kushikilia misimamo ya kulipa kwa awamu.
Taarifa zinaeleza kuwa Yanga waliwahi na kufunga dili hilo kwa kutoa ofa nono ambayo ilikubaliwa na mchezaji mwenyewe pamoja na klabu yake ya CS Sfaxien, Hii ni baada ya Rais wa Yanga kuingilia kati na kutuma ofa kubwa zaidi usiku wa jana, jambo lililopelekea pande zote mbili kuafikiana na kukamilisha dili mapema asubuhi hii.
Conte, ambaye alikuwa akiwaniwa na Simba pia, amehakikishiwa maslahi makubwa Yanga SC ikiwemo gari, nyumba ya kuishi, mshahara mnono, pamoja na nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza ofa ambayo imeonekana kumshawishi zaidi kuliko ile ya Simba.
Kwa upande wa Simba SC, chanzo cha ndani kimeeleza kuwa walikuwa tayari kuweka dau mezani lakini walitaka kulipa kwa awamu mbili, jambo lililokataliwa na CS Sfaxien ambao walisisitiza kulipwa fedha zote kwa mkupuo mmoja hali iliyoifanya Simba kushindwa kukamilisha usajili huo.
Wachambuzi wa soka wameanza kuhoji mbinu za Simba katika usajili wakisema ubahiri wa klabu hiyo unawagharimu sana, huku wapinzani wao wakifanikisha mikataba mizito bila kusuasua, Simba wanapaswa kubadilika. Kwenye soko la kisasa la usajili, klabu kubwa hailengi kubana matumizi kwenye wachezaji wa maana.
Kwa mafanikio haya ya Yanga, mashabiki wa klabu hiyo wamefurika mitandaoni wakipongeza uongozi kwa usajili huo wa kiwango, wakiamini kuwa Conte ataongeza nguvu kubwa kwenye safu ya kiungo kuelekea msimu mpya wa mashindano ya ndani na kimataifa.
0767915473.
lugembetimothy01@gmail.com.
Post a Comment