Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Mwekezaji wa klabu ya Simba SC, Mohammed Dewji maarufu kama Mo Dewji, amefichua kuwa hadi sasa ameshatumbukiza kiasi kikubwa cha fedha kinachofikia Shilingi Bilioni 87 katika klabu hiyo kongwe ya soka nchini ameyasema hayo siku ya Julai 14 , saa nne usiku.
Kupitia kurasa rasmi za mitandao ya kijamii za Simba SC na ukurasa wake binafsi, Mo Dewji ameeleza kuwa kati ya kiasi hicho, Bilioni 45 zilitumika moja kwa moja kwenye mishahara ya wachezaji, usajili pamoja na gharama nyingine za uendeshaji wa kila siku wa klabu.
“Nimewekeza Bilioni 20 katika miradi ya maendeleo ya klabu, na pia nimetumia Bilioni 22 ambazo hazijapitia mfumo rasmi, lakini zilitumika kwa maslahi ya klabu,” alisema Mo Dewji.
Mo Dewji pia alisisitiza dhamira yake ya kuendelea kuiwezesha Simba SC kuwa miongoni mwa klabu kubwa zaidi barani Afrika. “Nimetenga fedha za kutosha kuhakikisha timu yetu inakuwa bora zaidi. Kwa neema ya Mungu, Simba itajulikana kwa makubwa zaidi,” alisema kwa msisitizo.
Aliendelea kwa kusema kuwa mchango wake hautokani tu na fedha, bali pia ni wa moyo na mapenzi ya dhati kwa klabu hiyo. “Nimewekeza muda wangu, jasho, damu na fedha kwa ajili ya Simba, Ni klabu ninayoipenda kwa dhati,” aliongeza mfanyabiashara huyo maarufu.
Kauli hiyo imepokelewa kwa hisia tofauti na mashabiki wa Simba SC katika mitandao ya kijamii, wengi wakimpongeza kwa kujitoa kwake kwa hali na mali huku wakimwomba aendelee kusimama imara kwa ajili ya maendeleo ya klabu, huku wengine wakijiuliza pesa anazozitoa mwekezaji huyo Zina sura ipi?
Klabu ya Simba mpaka sasa imekuwa na sintofahamu tangu kumalizika kwa msimu bila ya kumaliza chochote lakini mwekezaji huyo amesema ataweka fedha nyingine kwaajili ya kuijenga timu imara kuelekea msimu ujao huku akisiaitiza umoja na mshikamano klabuni hapo.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.
Post a Comment