Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Bondia maarufu kutoka hapa nchini, Karim Mandonga, ameendelea kukumbwa na wakati mgumu kwenye ulingo baada ya kupoteza pambano lake dhidi ya Shaban Kaoneka kwa mara nyingine kupitia uamuzi wa pointi, katika Dar Boxing Derby iliyofanyika usiku wa kuamkia leo katika ukumbi wa Leaders Club, Dar es Salaam.
Katika pambano hilo lililokuwa na raundi sita lililokuwa la saba kwa usiku huo wa burudani ya ngumi, Mandonga alionyesha uthubutu wa hali ya juu kwa kumaliza raundi zote, mara baada ya hapo awali kuupoteza mapema bila kumaliza raundi , licha ya hivyo lakini hakuweza kuhimili makali ya mpinzani wake ambaye alionekana kumzidi maarifa na kasi ulingoni.
Shaban Kaoneka, ambaye amekuwa mwiba kwa Mandonga kwenye mapambano yao ya hivi karibuni, alithibitisha ubabe wake kwa mara nyingine kwa kutwaa ushindi kwa pointi na hii ni mara ya pili mfululizo baada ya kuandika kwa K'O mkoani Songea kwenye pambano lililopita. Mashabiki waliokuwepo Leaders Club walishuhudia raundi ya mwisho yenye ushindani na burudani ya hali ya juu, huku kila bondia akipigania heshima na ushindi.
Pambano hili lilikuwa sehemu ya mfululizo wa mapambano ya usiku huo yaliyosheheni burudani, na lilivuta hisia za mashabiki wengi wa masumbwi waliojitokeza kwa wingi kushuhudia vipaji na ushindani wa hali ya juu.
Pambano hili limekuwa ni dabi kwa mabondia Hawa na hiyo ni kutokana na tambo nyingi anazozitoa Mandoga nje ya uwanja kabla ya Pambano hali inayoleta ushindani ulingoni mpaka kwa wadau na Mashabiki wa mchezo wa masumbwi nchini.
Mashabiki sasa wanaendelea kusubiri kwa hamu kuona iwapo Mandonga atarejea kwa kishindo ama atafikiria njia mpya za kurejesha makali yake yaliyowahi kumpatia umaarufu mkubwa ndani ya nchi.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.
Post a Comment