Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Klabu ya Singida Black Stars imetangaza rasmi kumteua raia wa Argentina, Miguel Ángel Gamondi, kuwa Kocha Mkuu mpya wa kikosi hicho, kwa mkataba wa mwaka mmoja, kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya mwaka 2025/2026.
Kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na klabu hiyo, uongozi wa Singida Black Stars umeeleza kuwa uteuzi wa Gamondi ni sehemu ya mabadiliko muhimu katika benchi la ufundi, yaliyopitishwa na Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo kwa lengo la kuongeza ushindani na mafanikio msimu ujao.
Aidha, klabu hiyo imethibitisha kuwa Kocha David Ouma kutoka Kenya pamoja na Kocha Moussa N’Daw kutoka Senegal wataungana na Gamondi kama Makocha Wasaidizi, hatua inayoashiria kuundwa kwa benchi imara lenye uzoefu wa kimataifa.
Miguel Gamondi ni kocha mwenye uzoefu mkubwa barani Afrika, akiwa amewahi kufanya kazi na vilabu kadhaa vikubwa pamoja na timu za taifa, na sasa anakabidhiwa jukumu la kuipeleka Singida Black Stars kwenye mafanikio makubwa zaidi, ndani na nje ya nchi.
Mashabiki wa Singida Black Stars sasa wana matarajio makubwa kwa safu mpya ya benchi la ufundi, huku wakisubiri kwa hamu kuona mabadiliko hayo yakileta matokeo chanya ikiwemo kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.
Post a Comment