Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Katika juhudi za kuongeza uwazi na uelewa kwa mashabiki wa soka, Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limeanzisha utaratibu mpya ambapo waamuzi hutangaza maamuzi yao ya VAR moja kwa moja hadharani kwa kutumia kipaza sauti, tofauti na ilivyokuwa awali.
Kwa sasa, kila mara mwamuzi anapokwenda kutazama tukio kupitia teknolojia ya VAR, hutangaza uamuzi wake moja kwa moja kwa mashabiki waliopo uwanjani na pia kwa watazamaji kupitia runinga. Mabadiliko haya yameanza kutumika katika mashindano ya kimataifa kama Kombe la Dunia la Wanawake mwaka 2023 na pia Kombe la Dunia la Klabu linaloendelea mwaka huu nchini Marekani.
Hatua hii inalenga kuondoa mkanganyiko wa maamuzi ya VAR ambao umekuwa ukilalamikiwa kwa muda mrefu na wadau wa soka. Kupitia mfumo huu, mashabiki sasa wanaweza kuelewa sababu za msingi za maamuzi yanayofanywa na waamuzi katika matukio tata kama penalti, offsides, au madhambi ya kuchezea rafu.
“After review, no penalty accidental handball,” ni mfano wa maneno ambayo waamuzi sasa hutamka moja kwa moja uwanjani baada ya kutazama tukio kwa kutumia VAR.
Huku wakosoaji wakieleza kuwa bado kuna changamoto ya mawasiliano kwa mashabiki wanaotumia lugha tofauti, FIFA imesisitiza kuwa utaratibu huu ni hatua ya awali kuelekea soka lenye uwazi na haki zaidi, Inatarajiwa kuwa CAF na mashirikisho mengine ya kikanda barani Afrika nao wataanza kutumia mfumo hu kwenye mashindano makubwa kama AFCON na Ligi ya Mabingwa Afrika.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.
Post a Comment