TAIFA STARS YANG’ARA KWA KUITIMUA ESWATINI 2-1 KATIKA KOMBE LA COSAFA

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imeandika ukurasa mpya wa matumaini katika mashindano ya Kombe la COSAFA baada ya kuichapa Eswatini kwa mabao 2-1 katika mchezo wa kusisimua uliopigwa jana kwenye Uwanja wa Free State, Bloemfontein nchini Afrika Kusini.

Katika mchezo huo Eswatini walikuwa wa kwanza kuliona lango dakika ya 29 kupitia kwa mshambuliaji wao hatari Andy Junior Magagula, aliyeunganisha vyema pasi safi na kuipatia timu yake bao la kuongoza.

Hata hivyo, vijana wa Kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ hawakutetereka, Walirejea mchezoni kwa kasi na kufanikiwa kusawazisha dakika ya 37 kupitia kwa kiungo mahiri Iddy Seleman Nado aliyeachia kombora kali lililomshinda mlinda mlango wa Eswatini.

Kipindi cha pili kilishuhudia Taifa Stars wakiongeza kasi ya mashambulizi huku wakitawala eneo la kati, Jitihada zao zilizaa matunda dakika ya 69 baada ya Shekhani Khamis kufunga bao la ushindi kwa ustadi mkubwa, akimalizia mpira wa kona uliopigwa kwa ustadi na winga George Mpole.

Akizungumza baada ya mechi, Kocha Hemed alisema ushindi huo ni matokeo ya maandalizi mazuri na ari ya juu ya wachezaji wake. “Tumekuwa tukijenga timu kwa muda na sasa tunaanza kuona matunda. Ushindi huu ni muhimu sana kwa kujenga morali kuelekea mechi zijazo,” alisema.

Kwa matokeo hayo, Tanzania sasa inashika nafasi ya pili katika kundi C ikiwa na pointi tatu, na inabaki na matumaini ya kufuzu hatua ya mtoano endapo itafanya vizuri katika mchezo wake ujao, Kwa upande mwingine, Eswatini wamesalia na pointi moja tu na nafasi yao ya kuendelea katika mashindano haya inaonekana kuwa finyu.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments