RONALDO ANAZEEKA UTAMU UNAZIDI

Na Timothy Lugembe

Mwanakwetu Sports

Wakati wengi wakifikiri umri ungemweka kando, Cristiano Ronaldo anaendelea kuwa kivutio kikuu katika ulimwengu wa soka, Akiwa na miaka 40 sasa, Ronaldo bado anaonesha kiwango cha juu uwanjani, akiwapa changamoto vijana waliotoka shule jana! Katika dunia ambayo kasi na nguvu vinahitajika zaidi, Ronaldo amegeuka kuwa somo hai la nidhamu, bidii na mapenzi ya kweli kwa mpira.

Kipenzi hiki cha mashabiki kutoka Ureno, ambaye amewahi kutamba katika vilabu vikubwa kama Sporting Lisbon, Manchester United, Real Madrid, Juventus, na sasa Al Nassr ya Saudi Arabia, amejikusanyia tuzo zisizohesabika.

Hadi kufikia sasa, Ronaldo amefunga magoli 937 ya mashindano rasmi, akivunja rekodi ya dunia ya mfungaji bora wa muda wote. Mbali na hayo, ana tuzo 5 za Ballon d’Or, na ameongoza timu ya taifa ya Ureno kutwaa ubingwa wa Euro 2016 na UEFA Nations League 2019  na sasa kaifikifa Timu yake fainali mashindano ya UEFA nations league.

Ukweli ni kwamba, Ronaldo si tu mchezaji, bali ni chapa inayovutia   ndani na nje ya uwanja, Anapocheza, heshima na hofu hutawala, Kila mkwaju wake wa kona ni tishio, kila mkwaju wa penalti ni historia mpya, na kila dakika anapokanyaga uwanja ni somo kwa kizazi kinachokuja.

Ingawa kasi yake ya miaka 20 imepungua kidogo, akili yake ya mpira imekuwa kali zaidi. Anaongoza kwa uzoefu, anaongoza kwa matokeo, na anaendelea kuvutia mamilioni kwa staili yake ya kipekee ya uchezaji.

Wengine wanazeeka na kusahaulika, lakini Ronaldo anazeeka na kutukuzwa, Utamu wake hauishi ni kama divai ya gharama, inavyozidi kukaa, ndivyo inavyozidi kuwa tamu, na hadi leo, Cristiano Ronaldo bado ni jina linalotikisa, si tu kwa mashabiki bali hata kwa wapinzani.



0/Post a Comment/Comments