MZEE WA UMRI KIJANA UWANJANI, AIONGOZA PORTUGAL KUTWAA UBINGWA MBELE YA SPAIN

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Katika usiku wa kipekee ulioweka historia mjini Munich, Ureno waliibuka mabingwa wa UEFA Nations League kwa mara ya pili baada ya kuichapa Uhispania kwa mikwaju ya penalti 5–3, kufuatia sare ya mabao 2–2 ndani ya dakika 120 katika uwanja wa Allianz arena Munich nchini ujerumani.

Mchezo huu wa kusisimua ulikuwa wenye kuvutia, ukiwa ni fainali ya kukumbukwa kwa hisia, uhodari na hadithi ya mwisho ya gwiji Cristiano Ronaldo, Uhispania walionekana kutawala mapema kwa mabao ya Martín Zubimendi na Mikel Oyarzabal, wakionyesha soka la hali ya juu. Hata hivyo, Ureno walikataa kukata tamaa ,Nuno Mendes aliwapatia bao la kwanza kabla ya nahodha wao, Cristiano Ronaldo, kusawazisha kwa ustadi wa kipekee na kuleta shangwe kwa mashabiki wa Seleção.

Baada ya dakika za kawaida na za nyongeza kuisha bila mshindi, mchezo uliamuliwa kwa mikwaju ya penalti. Álvaro Morata wa Hispania alikosa mkwaju wa penati na shukrani ikawa kwa kipa Diogo Costa aliyeokoa kwa ustadi, kabla ya Rúben Neves kuhitimisha kwa penalti ya ushindi iliyowatumbukiza mashabiki wa Ureno katika bahari ya furaha.

Cristiano Ronaldo, mwenye umri wa miaka 40, alicheza mechi yake ya fainali ya kimataifa kwa fahari kubwa, Aliondoka uwanjani kwa machozi ya furaha, akiwa ameandika ukurasa wa hadithi yake ya kipekee ya taifa kwa taji jingine mikononi, akiwa mchezaji mzee zaidi kufunga katika fainali ya UEFA Nations League.

Kwa ushindi huo, Portugal wameweka rekodi mpya kama taifa la kwanza kushinda UEFA Nations League mara mbili (2019 na 2025). Fainali hii haikuwa tu pambano la taji, bali pia tamthilia ya uzalendo, ujasiri, na mwisho wa enzi ya Ronaldo iliyojaa heshima na shangwe.



0767915473

lugembetimothy01@gmail.com.

0/Post a Comment/Comments