MNYAMA ATAUNGURUMA TENA

 


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Katika jangwa la changamoto, ambapo upepo wa lawama huvuma mithili ya kimbunga na nyota hung’aa kisha kufifia, Simba Sports Club imesalia kuwa taa isiyozimika, taa iliyowasha moto wa soka la Tanzania na kujitangaza mpaka nje ya mipaka ya Afrika.

Ni kweli, Simba amekumbwa na dhoruba za hivi karibuni kushindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, kutoka mapema kwenye mashindano ya CAF, na misukosuko ya kiuongozi, Lakini hata mawe yakipigwa na mvua, hayapotezi thamani yake. Simba ni jiwe la msingi, si jani linalopeperushwa na upepo.

Simba si klabu tu; ni sauti ya mtaa, ni kishindo cha uwanja, ni damu ya mashabiki wake wanaolia na kucheka pamoja, Timu hii imeshika mkono wa soka la Tanzania na kulivusha barabara ya vumbi hadi kwenye njia ya lami, Nani asiyekumbuka mwaka 2019 hadi 2021, Simba alipoiteka Afrika, akiwatoa vigogo kama AS Vita na Al Ahly? Ilikuwa si hadithi tu, bali uhalisia uliotupa fahari ya kuwa Watanzania.

Wakati wengine walikuwa wakijifunza kutembea, Simba alikuwa akikimbia na kupeperusha bendera ya nchi kwenye jukwaa la kimataifa. Alikuwa kama simba wa jangwani mnyenyekevu akiwa kimya, lakini mkali akiwa kazini.

Kama ngoma ya asili, mchezo wa Simba una mapigo yenye ladha ya Kiafrika pasi fupi za haraka kama mshale wa mkulima, mipira mirefu ya kiufundi kama nyimbo za harusi za Kisukuma, Simba alivutia wachezaji wakubwa kuja nchini kina Clatous Chama, Meddie Kagere, Luis Miquissone ambao walicheza kama ndoto yenye uhalisia.

Simba aliwasha moto katika mioyo ya vijana, akaamsha ndoto zilizokuwa zimelala, Leo hii, kijana wa Mtwara anaota kuwa beki wa Simba, msichana wa Mwanza anaamini anaweza kuwa kocha wa timu ya taifa kwa sababu Simba aliweka mfano. Mti wa Simba umetanda mizizi kwenye ardhi ya Tanzania, na matunda yake yameanza kuiva si kwenye kikapu cha ubingwa tu, bali kwenye mabadiliko ya fikra, nidhamu, na ufanisi.

Ushujaa wa kweli haupimwi kwa idadi ya mapambano aliyoshinda, bali kwa uwezo wa kusimama baada ya kuanguka. Simba amedondoka, lakini hajafa, Kila jeraha kwake ni alama ya historia, kila tone la jasho ni ushahidi wa mapambano. Leo hii, klabu inajitathmini, inajipanga upya, na bila shaka itarudi si kama simba wa porini, bali kama simba aliyevaa taji.

Katika makaa ya changamoto ndipo almasi hung’aa. Simba ni mfano hai wa msemo huu. Ni simba aliyejeruhiwa, lakini mwenye macho yanayowaka tamaa ya kulinda hadhi, kulipiza kisasi cha kimichezo, na kuandika sura mpya ya ushindi.

Wakati wa Kuandika Upya Hadithi Kwa watani wa jadi, huenda ni muda wa kucheka. Kwa mashabiki wa Simba, ni muda wa kuamka na kuamini tena, Historia haipotei hujificha tu ili ijitokeze kwa kishindo. Simba hawezi kufa; anaweza kuchoka, anaweza kunyamaza kwa muda, lakini siku atakapoamka, dunia itasikia Kwa sababu, simba halalamiki huinamisha kichwa, huvuta pumzi, na kurudi vitani akiwa mkali zaidi.

Na tunaposema “Mnyama anaamka,” hatuzungumzii manyoya bali moyo, si mluzi bali mioyo ya mamilioni ya walio tayari kusimama nyuma ya rangi nyekundu na nyeupe.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments