IBENGÉ KUJIUNGA NA AZAM FC,MAKUBWA YATARAJIWA

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports,

Klabu ya Azam FC ipo mbioni kumtangaza rasmi kocha mahiri raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Florent Ibengé, kuwa Kocha Mkuu mpya wa kikosi hicho, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuimarisha timu kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa akitokea Al hilal ya sudani.

Taarifa kutoka vyanzo vya karibu na klabu hiyo zinaeleza kuwa tayari makubaliano kati ya pande hizo mbili yamefikiwa, huku Ibengé akitarajiwa kuwasili nchini hivi karibuni kwa ajili ya utambulisho rasmi, Hatua hii imekuja kufuatia tathmini ya ndani inayofanywa na uongozi wa Azam FC kuhusu mwenendo wa kikosi hicho na mafanikio yaliyokosekana msimu uliopita.

Florent Ibenge ni jina kubwa kwenye ramani ya soka barani Afrika. Aliwahi kuiongoza timu ya taifa ya DR Congo kwenye mashindano ya CHAN mwaka 2016 na kuifikisha hatua ya juu kwenye AFCON. Pia ameinoa AS Vita Club, RS Berkane ya Morocco, na hivi karibuni klabu ya Al Hilal ya Sudan, akifanikiwa kutwaa mataji mbalimbali.

Ujio wa Ibenge unatazamwa kama hatua ya kimkakati kwa Azam FC, ambao wameonesha nia ya kweli ya kurejea katika ubora wao wa juu, wakilenga si tu ushindani wa ndani bali pia mafanikio kwenye michuano ya CAF.

Hadi sasa, bado uongozi wa Azam haujatoa tamko rasmi, lakini wadau wa soka nchini wameshaanza kuonesha matumaini mapya, wakiamini kuwa Ibenge anaweza kuwa chachu ya mabadiliko makubwa ndani ya kikosi hicho kinachomilikiwa na Kampuni ya Bakhresa.



0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments