CLEMENT MZIZE KARIBU KUVAA JEZI YA ZAMALEK! YANGA YASUBIRI MALIPO KUKAMILISHA DILI LA KIHISTORIA


Na Timothy Lugembe

Mshambuliaji machachari wa Yanga Africa , Clement Mzize, yuko mbioni kutimkia kwenye klabu kongwe ya Zamalek SC ya Misri baada ya pande zote mbili kukubaliana kuhusu masharti ya uhamisho huo mkubwa, ambao unatajwa kuwa miongoni mwa dili nono zaidi kwa mchezaji kutoka Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa leo na The Citizen, mazungumzo kati ya Yanga na Zamalek yamefikia hatua ya mwisho huku kinachosubiriwa kwa sasa kikiwa ni malipo kutoka kwa mabingwa hao wa Afrika Kaskazini ili uhamisho huo ukamilike rasmi.

“Tumeshakubaliana na Zamalek kuhusu masharti ya uhamisho wa Mzize. Wamekubali, lakini bado hawajafanya malipo. Tunawasubiri wakamilishe malipo ili dili likamilike,” kilisema chanzo kutoka ndani ya Yanga kilichozungumza kwa masharti ya kutotajwa jina.

Mzize, ambaye msimu huu amefunga mabao 13 na kusaidia mengine matatu, ameonekana kuwa lulu inayowindwa na vilabu mbalimbali kutokana na kiwango chake cha juu akiwa na Wananchi.

Iwapo dili hilo litakamilika, litamfungulia mlango mkubwa Mzize katika soka la kimataifa, huku pia likiiingizia Yanga fedha muhimu kwa mipango ya kuimarisha kikosi chake msimu ujao.

Kwa sasa macho yote yanaelekezwa kwenye makao makuu ya Zamalek huko Cairo  je, wataweka mezani fedha hizo kukamilisha dili au kutakuwa na mabadiliko ya dakika za mwisho?

 

0/Post a Comment/Comments