Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Mashindano ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara msimu huu yamechukua sura ya kipekee, huku vita ya kuwania tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu ikionekana kuchukua mwelekeo mkali kati ya nyota wawili wanaong’ara Ahoua Charles wa Simba SC na Pacôme Zouzoua wa Yanga SC.
Kwa upande wa Ahoua Charles, ameonesha kiwango cha juu akiongoza orodha ya wafungaji bora kwa kufunga mabao 16, Si tu kwamba ni mfungaji mahiri, bali pia ni mchezaji mwenye uwezo wa kutoa pasi za mwisho, akiwa nafasi ya pili kwenye orodha ya watoa pasi za mabao (assists) akiwa na jumla ya pasi 9, Uwezo huu wa kuchangia mabao kwa njia mbili unamuweka katika nafasi nzuri ya kushinda tuzo hiyo.
Kwa upande mwingine, Pacôme Zouzoua naye ameonesha kiwango cha kuvutia akiwa na mabao 11 na pasi 8 za mabao, Ingawa hakuwa kinara wa mabao au pasi, Zouzoua amekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya Yanga SC, akionesha uwezo wa kucheza kwa kiwango cha juu katika mechi muhimu na kuisaidia timu yake kupata matokeo mazuri.
Takwimu hizi zinaonyesha kuwa wawili hawa ni washindani wa kweli, Ahoua amekuwa hatari katika safu ya ushambuliaji, wakati Zouzoua ameonesha ubunifu mkubwa katika dimba la kati. Mashabiki wa soka nchini sasa wanatazama kwa hamu uamuzi wa mwisho wa TFF kuhusu nani ataibuka na tuzo hiyo ya heshima huku takwimu zikimbeba zaidi Ahoua.
Je, ni Ahoua Charles wa Simba SC atakayeibuka kidedea kwa uwezo wake mkubwa wa kufumania nyavu? Au ni Pacôme Zouzoua wa Yanga SC kwa mchango wake wa pande zote mbili za ushambuliaji? Muda ndio utakaotoa majibu Mashabiki wanasubiri kwa shauku kubwa kutangazwa kwa Mchezaji Bora wa NBC Premier League msimu huu.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.
Post a Comment