Na Timothy Lugembe
Mwanakwetu Sports
Kwenye mafanikio ya kila mmoja, lazima huwa kuna msaada anaopata kutoka kwa watu walioko nyuma yake. Inaweza kuwa kimawazo, kifedha au kupitia mitandao ya kijamii. Hatuwezi kuyataja mafanikio ya mchezaji nyota kwa sasa ulimwenguni, Lamine Yamal, bila kuwataja miamba miwili, yaani Lamine na Yamali.
Kabla ya kuzaliwa kwa mtoto Lamine Yamal, familia yake ilikuwa ikipitia changamoto za kiuchumi, hali iliyosababisha wazazi wake kutafuta msaada nje ili kuweza kufanikisha ukuaji wa mtoto huyo. Mzee Nasraoui, baba mzazi wa kinda huyo ambaye alijishughulisha na upigaji rangi, hakufanikiwa kupata kipato kwa ajili ya kumlea mtoto wake na badala yake aliamua kwenda moja kwa moja kutafuta msaada kwa ndugu na jamaa wa karibu.
LAMINE
Mtu huyu alichangia ukuaji wa Lamine Yamal baada ya kutoa msaada wa vitu vya nyumbani ikiwemo vyakula, maji pamoja na mahitaji mengine. Baada ya kutoa msaada huo, Mzee Nasraoui, baba wa Lamine Yamal, aliahidi kuwa pindi mtoto atakapozaliwa atamuita Lamine kama heshima na kuthamini msaada wa mtu huyo.
YAMALI
Ni mtu aliyeshiriki kulipia kodi ya nyumba wakati wa kipindi kigumu alichokuwa anapitia Mzee Nasraoui, na baada ya msaada huo aliahidi tena kuwa pindi mtoto atakapozaliwa atamuita Yamali kama heshima na kutambua msaada huo.
Baada ya kuzaliwa kwa mtoto, wazazi wake waliamua kumpatia jina la Lamine Yamal kama heshima kwa watu waliofanikisha harakati za kuzaliwa kwake, ambapo hata maana ya majina hayo yamezidi kuwa baraka na mafanikio kwa kinda huyo. Uaminifu na uzuri ndiyo maana halisi ya jina hilo kutoka kwenye kamusi za lugha ya Kiarabu.
Alizaliwa tarehe 13 Julai 2007 katika mji wa Esplugues de Llobregat, karibu na Barcelona. Yamal ana asili ya Kihispania kupitia mama yake na asili ya Kiequatorial Guinea kupitia baba yake.
Yamal alijiunga na akademia maarufu ya FC Barcelona, La Masia, akiwa na umri wa miaka sita. Alionyesha maendeleo ya haraka, akipanda ngazi kupitia vikundi vya umri kwa kasi isiyo ya kawaida. Mnamo Aprili 29, 2023, akiwa na umri wa miaka 15 na siku 290, alifanya historia kwa kuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kuchezea timu ya kwanza ya Barcelona katika ushindi wa 4-0 dhidi ya Real Betis.
Lamine Yamal anaonekana kuwa mmoja wa vipaji vikubwa zaidi katika soka la kisasa. Kwa mafanikio yake ya mapema na uaminifu kwa klabu yake, mpaka sasa amefanikiwa kutwaa vikombe tofauti tofauti. Ijapokuwa akiwa na umri mdogo, ametwaa kombe la Ligi nchini Hispania, ametwaa ubingwa wa Euro, ametwaa Kombe la Mfalme, na msimu huu ameifikisha timu yake ya FC Barcelona hatua ya nusu fainali ya mashindano ya UEFA. Hivyo, anatarajiwa kuwa mchezaji wa kipekee katika historia ya FC Barcelona na soka la dunia kwa ujumla.
Hivyo, shukurani za dhati ziende kwa Lamine na Yamali kwa upendo na huruma yao kwa kufanikisha kuzaliwa kwa Lamine Yamal, kinda ambaye mpaka sasa jina lake linaimbwa kote ulimwenguni. Hivyo basi, katika haya maisha usimkatie mtu tamaa—toa msaada inapohitajika, kwani ni hazina kwa siku za baadaye.
lugembetimothy01@gmail.com
0767915473
Post a Comment