Yanga: Hawa Marumo tunao

 

RUTENBURG. Ni mechi inayoonekana kuwaunganisha Watanzania wengi hapa Afrika Kusini ambapo wameonekana kuweka kando tofauti za Usimba na Uyanga ambazo zimezoeleka kwa wapenzi wa timu hizo mbili na kuipa sapoti Yanga ili kupata matokeo mazuri yatakayoivusha na kuipeleka katika nusu fainali.

Kwa kinachoendelea hapa viongozi wa Yanga wamesema njia ya kupata ushindi inaonekana na sapoti ni kubwa huku mashabiki wengi kwenye mitandao ya Yanga wakitaka Clement Mzize na Fiston Mayele waanze katika kikosi cha leo.

Kundi kubwa la Watanzania lilijitokeza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo kuipokea na kuilaki Yanga huku baadhi wakiwa wamevaa jezi za timu hiyo, wengine wakivaa za Simba na wapo waliovaa jezi zilizoandikwa Tanzania.

Mfano mwingine wa hilo ni Mtanzania, Swalehe Madjapa ambaye amesafiri kutoka Tanzania hadi Afrika Kusini kuisapoti Yanga huku akiwa ni mwanachama na shabiki wa Simba.


VIGOGO KIBAO, WATAMBA
Msafara wa Yanga Afrika Kusini umehusisha kundi kubwa la viongozi wa serikali na wadau wa timu hiyo hasa wale wenye uwezo wa kifedha kwa lengo linaloonekana kwenda kuipa hamaa timu hiyo ili iweze kutinga hatua ya fainali ya mashindano hayo.

UWANJA WA YANGA MTEGO
Mechi hiyo imepangwa kuchezwa katika Uwanja wa Royal Bafokeng ambao Marumo imeutumia kwa mechi zake mbili kati ya tano zilizopita za Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga inapaswa kufanya kazi ya ziada kumaliza ubabe wa Marumo Gallants kwenye Uwanja huo kwani timu hiyo ya Afrika Kusini, imeshinda mechi zake zote mbili ilizocheza uwanjani hapo dhidi ya Al Ahli Tripoli na Pyramids FC, imeshinda zote bila kuruhusu bao na imepachika mabao manne.
Kimsingi Marumo Gallants sio timu rahisi inapokuwa nyumbani kwa vile katika mechi zote tano za mashindano hayo ilizocheza nyumbani, imeshinda zote, imefunga mabao 13 na kuruhusu nyavu zakekutikiswa mara tatu.

Royal Bafokeng ni miongoni mwa viwanja 10 vilivyotumika katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Afrika Kusini mwaka 2010 ambapo uliandaa idadi ya mechi sita, tano zikiwa za hatua ya makundi na moja ikiwa ni ya raundi ya 16 bora.

Ni uwanja wa nyasi za kawaida uliofunguliwa rasmi mwaka 1999 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2009 huku ukiwa unaingiza idadi ya mashabiki 44,530.
Suala la chakula halionekani kama ni changamoto kwa Yanga hapa Afrika Kusini kwani vyakula vingi vilivyozoeleka nyumbani Tanzania, vinapatikana hapa.

Chakula kinachopendelewa zaidi na Watanzania hapa ni wali lakini pia kuna ugali na mboga za nyama, samaki, maini na zile za majani nyingi zilizopo Tanzania zinapatikana hata huku.

Ulipotua Johannesburg, ulipokelewa na Balozi wa Tanzania nchini humo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi pamoja na maofisa wa ubalozi kutokea Pretoria ambako upo.
Kutoka nyumbani, upande wa serikali unaongozwa na Naibu Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Hamis Mwinjuma lakini pia kwa upande wa Yanga, mdhamini na mfadhili wa timu hiyo, Bilionea Ghalib Said Mohammed (GSM) ni miongoni ataongoza kundi la vigogo wa timu hiyo waliopo hapa.
Yanga mjini Rutenburg wamefikia katika hoteli ya Royal Marang ambayo gharama ya chini ya chumba kimoja ni Randi 2140 (Sh 264,900).

Hoteli hiyo mbali ya kuwa na kumbi ya gym ya kisasa kwa ajili ya mazoezi, ina mabwawa ya kifahari ya kuogelea, viwanja vya kisasa vya michezo ya mpira wa wavu na tenisi lakini pia ina kumbi za michezo ya kompyuta.
Kuna kumbi tano kubwa na za kifahari za mikutano katika hoteli hiyo iliyopo jijini Rusternburg. Kwa kukaa katika hoteli hiyo tangu jumapili hadi siku ya mchezo, Yanga itakuwa imetumia zaidi ya Sh 100 milioni kwa gharama za malazi, chakula na nyinginezo.
Rusternburg ambako hoteli hiyo ya Royal Marang ipo, lipo Kaskazini Magharibi mwa jiji maarufu la Afrika Kusini la Johannesburg na makao makuu ya nchi hiyo, Pretoria.

0/Post a Comment/Comments