Bangala amkaushia Ibenge


 

KIRAKA wa Yanga, Yannick Bangala, amevunja ukimya na kuwatumia salamu mashabiki wa klabu hiyo kuwa, iwe isiwe ni lazima chama lao litinge makundi, huku akimfungia vioo kocha wake wa zamani, Florent Ibenge anayeinoa Al Hilal ya Sudan.

Bangala alisema, licha ya kujua ubora wa Kocha Ibenge, lakini safari hii itakula kwake kwa vile Yanga imepania jambo moja tu, kupata matokeo mazuri kwenye mchezo wao wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika ili kutinga makundi kuyasaka mamilioni ya fedha yaliyopo kwenye michuano hiyo.

Nyota huyo kutoka DR Congo, ambaye ubora wake uwanjani wa kucheza nafasi nyingi na kupewa jina la Mzee wa Kazi Chafu, aliliambia Mwanaspoti, kitu kilichopo akilini mwa wachezaji ya Yanga ni kutinga makundi mbele ya Al Hilal ya Sudan watakaovaana wikiendi ijayo.

Bangala alisema wanafahamu baadhi yao waliwahi kufanya kazi na Kocha Ibenge, lakini safari hii watakapokutana itabidi awasamehe tu.

“Tunafahamu kama wachezaji kuwa mara ya mwisho Yanga kucheza makundi katika Ligi ya Mabingwa ni mwaka 1998, tunataka kuirudisha timu hatua hiyo,” alisema Bangala ambaye alichukua tuzo ya Mchezaji Bora wa msimu uliopita Yanga ikichukua makombe matatu bila kupoteza.

“Tunajua haitakuwa kazi rahisi, tunakutana na timu nzuri inayofuindishwa na kocha aliyetulea tunamheshimu sana na alitulea kama watoto wake lakini kwa kukutana naye ni jambo la kawaida kwenye mpira, hatuwezi kuweka malengo yetu pembeni kwa kuwa tumekutana na kocha aliyetulea ili atufunge hapana, tutapambana tuingie hatua ya makundi,” alisisitiza Bangala na kuongeza jeuri ya kuitoa Al Hilal inatokana na aina ya kikosi walichonacho msimu huu ambapo ongezeko la wachezaji wapya pamoja na wao waliokuwepo tangu msimu uliopita ndio mtaji mkubwa kwao.

Alisema Yanga pia ina kocha bora Nasreddine Nabi ambaye watatumia mbinu zake kushinda mbele ya Ibenge watakapokutana Oktoba 8 katika mchezo wa kwanza utakapigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kabla ya kurudiana nao wiki moja baadaye mjini Khartoum, Sudan.

“Imani yangu inatokana na wachezaji ambao wameongezeka msimu huu ni wazuri sana wameongeza kitu kikubwa ndani ya timu na kuifanya kuwa bora zaidi. Akili yetu sasa ni kwa hawa Al Hilal ambao ndio kizingiti kilichopo mbele yetu na kwa timu tuliyonayo tunaweza kuwatoa,” alisema na kuongeza:

“Najua Kocha Ibenge anatujua baadhi yetu hapa lakini sisi tutatumia mbinu za kocha wetu Nabi kupata matokeo. Tunajua Al Hilal ina wachezaji wazuri lakini hatuwezi kumuangalia mchezaji mmoja pekee kupata matokeo tutaweka umakini kwa kuiangalia timu yao nzima.”

 

 

 


0/Post a Comment/Comments