Alama moja kuwavusha Wananchi kwenda robo fainali


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Klabu ya Yanga imefanikiwa kutinga hatua ya makundi ya Ligi Mabingwa Afrika kwa mara ya nne mfululizo, huku ikiwa na kumbukumbu ya alama moja iliyowanyima nafasi ya kuvuka hatua ya makundi na kutinga robo fainali katika misimu miwili iliyopita.

Katika misimu mitatu iliyopita ambayo wamecheza hatua ya makundi, Yanga imefanikiwa kuvuka kwenda robo fainali mara moja kwenye msimu wa 2023/24, baada ya kukusanya alama nane na kumaliza nafasi ya pili nyuma ya Al Ahly iliyokuwa kinara kwa alama 12.

Katika misimu miwili iliyofuata, klabu hiyo ilishindwa kuvuka hatua ya makundi baada ya kumaliza ikiwa na alama nane katika kila msimu. Msimu wa 2024/25 walimaliza nafasi ya tatu nyuma ya MC Alger iliyokusanya alama tisa, huku msimu wa 2025/26 wakimaliza pia nafasi ya tatu, nyuma ya AS FAR Rabat iliyokuwa na alama tisa.


Kwa misimu yote mitatu iliyopita, Yanga imekuwa ikikusanya alama nane kila msimu. Hali hiyo inaonyesha kuwa tofauti ya alama moja imekuwa kikwazo katika safari yao ya kwenda robo fainali katika misimu miwili iliyopita.

Moja ya maeneo ambayo Yanga inahitaji kuboresha ni matumizi ya uwanja wa nyumbani, ambako ilishindwa kukusanya alama zote tisa, endapo wataongeza juhudi na kupata angalau alama moja zaidi ya zile walizokuwa wakikusanya katika misimu iliyopita, wanaweza kuongeza nafasi ya kuvuka hatua ya makundi na kuendelea na safari ya kutafuta taji hilo.

Msimu wa 2026/27, Yanga imepangwa Kundi B pamoja na Zamalek ya Misri, MC Alger ya Algeria na Club Africain ya Tunisia. Kundi hilo linaonekana kuwa na ushindani, lakini pia lina nafasi kwa Yanga kupata matokeo.


Timu hizo za Afrika Kaskazini zinapokutana, mara nyingi michezo yao huwa na ushindani mkubwa, hali inayoweza kufanya iwe vigumu kwa timu moja kupata alama zote tisa katika michezo yake ya nyumbani ambapo, Yanga inaweza kutumia vizuri michezo yake dhidi ya wapinzani hao kupata alama muhimu, hasa inapocheza nyumbani.

Hivyo, Yanga inahitaji kuhakikisha inavuna angalau alama tisa na zaidi ikiwa ni ongezeko la alama moja na zaidi kutoka katika misimu mitatu iliyopita. Hatua hiyo inaweza kuwa muhimu katika kufanikisha lengo la kuvuka hatua ya makundi na kutinga robo fainali, bila kujali ugumu wa kundi ililopangwa.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments